Imeandikwa na Fransisca Emmanuel
WAKILI wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga ameieleza Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa amepata taarifa kutoka kwa
daktari wa Magereza kwamba mfanyabiashara Yusuf Manji (41), amepelekwa
katika Hospitali ya Gereza la Keko kwa kuwa hali yake sio nzuri.
Katuga alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi
kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa jana. Alidai Manji ameshindwa
kufika mahakamani hapo kwa kuwa anaumwa na amepelekwa hospitalini hapo
kwa ajili ya matibabu na kwamba washitakiwa wengine wapo.
Mbali na Manji, washitakiwa wengine ni Meneja Rasilimaliwatu wa
Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda (28), Mtunza stoo,
Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43), mkazi wa Chanika
wanakabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi.
Aidha, Katuga alidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika, lakini
upo katika hatua za mwisho. Wakili wa washitakiwa, Hudson Ndusyepo
alidai hawana shaka na lililoongelewa na upande wa mashitaka lakini wa
naomba upelelezi ukamilike.
Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 4 mwaka huu kwa ajili
ya kutajwa. Inadaiwa Juni 30, mwaka huu maeneo ya Chang’ombe A wilayani
Temeke Dar es Salaam, washitakiwa wote kwa pamoja, walikutwa na askari
polisi wakiwa na mabalo 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare
za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vyenye thamani ya Sh milioni
192.5.
Pia inadaiwa Julai mosi mwaka huu, maeneo ya Chang’ombe A, wilayani
Temeke, Dar es Salaam, washitakiwa wote walikutwa na askari polisi
wakiwa na mabalo nane ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za
JWTZ vyenye thamani ya Sh milioni 44.
Katika mashitaka ya tatu, inadaiwa Juni 30, mwaka huu maeneo ya
Chang’ombe A, washitakiwa walikutwa wakiwa na mhuri wa JWTZ ambao
uliandikwa ‘Mkuu wa Kikosi 121 Kikosi cha JWTZ’ bila kuwa na uhalali
kitendo kinachohatarisha usalama wa nchi.
Pia inadaiwa, terehe hiyohiyo maeneo ya Chang’ombe washitakiwa
walikutwa na mhuri uliokuwa umeandikwa ‘Kamanda Kikosi 834 KJ Makutupora
Dodoma’ bila kuwa na uhalali kitendo kinachohatarisha usalama.
Ilidaiwa Juni 30, mwaka huu, maeneo hayo, washitakiwa kwa pamoja
walikutwa na mhuri ulioandikwa ‘Commanding Officer 835 KJ, Mgambo P.o.
Box 224 Korogwe’ isivyo halali. Katika mashitaka ya sita, inadaiwa Julai
Mosi mwaka huu, maeneo hayo ya Chang’ombe, washitakiwa walikutwa na
gari lenye namba za usajili SU 383 mali waliyojipatia isivyo halali.
Aidha, wanadaiwa kuwa Julai Mosi mwaka huu, maeneo ya Chang’ombe A
wilayani Temeke, Dar es Salaam, washitakiwa wote walikutwa na gari lenye
namba za usajili SM 8573 pasipo uhalali.
Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa sheria ya uhujumu
uchumi na ya usalama wa Taifa haijaipa mamlaka mahakama kusikiliza kesi
hiyo. Upande wa mashitaka ulidai wamepata hati ya kupinga dhamana kutoka
kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuomba washitakiwa wasiruhusiwe
kupewa dhamana kwa sababu wakiachiwa watahatarisha usalama na maslahi ya
nchi. Pia alidai kwenye mashitaka ya kwanza na ya pili, Mahakama ya
Kisutu haina mamlaka ya kushughulikia masuala ya dhamana.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment