Thobias Robert - MAELEZO
Wanawake
wa Jumuiya ya Tanzania Fellowship of churches kutoka makanisa
mbalimbali wanatarajia kufanya kongamano la maombi na dua maalumu
kwaajili ya kumuombea ulinzi Rais Dkt. John Magufuli kwa kazi nzuri
anayoifanya katika kutetea wanyonge na kulinda rasilimali za nchi.
Hayo
yamesemwa leo, Jijini Dar es Salaam na Mratibu wa kongamano hilo
Mchungaji Deborah Malassy, wakati akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu kongamano hilo la siku tatu linalotarajia kuanza Julai 20 hadi Julai 23 mwaka huu katika ukumbi wa Millenium Tower ulioko Jijini humo.
Mchungaji
Malassy amesema kuwa, kongamano hilo linalenga kutoa shukrani kwa
Mwenyezi Mungu kwa kuipatia Nchi ya Tanzania Kiongozi ambaye Watanzania
walikuwa wanamhitaji kwa muda mrefu ili kulinda amani ya Nchi, kutetea
wanyonge pamoja na kusimamia rasilimali za nchi pamoja na uadilifu
kazini.
“Mwaka
huu, ni mwaka wa Baraka na Neema kwa Taifa la Tanzania kufuatia matendo
makuu ya Mungu aliyotutendea Watanzania, hasa kuwa na kiongozi mwenye
uwezo, mcha Mungu, mtiifu mkweli na asiyependa mapato ya Serikali
kupotea,” amesema Mchungaji Malassy.
Aidha
amesema, kwa muda mfupi aliokaa madarakani, Rais Magufuli amefanya
mambo mengi na kila Mtanzania ameyashuhudia kama vile kurejesha maadili
kwa watumishi wa Umma, kuwaondoa viongozi wala rushwa pamoja na kutetea
rasilimali za Tanzania zilizokuwa zikisafirishwa nje ya nchi, mfano
mchanga wa dhahabu.
Vile vile kongamano hilo litatoa elimu kwa wanawake juu ya kujilinda
dhidi ya unyasasaji wa kijinsia, na kuwajengea Wanawake uwezo wa namna
ya kujikwamua kiuchumi pamoja na kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia
unaotokana na rushwa ya ngono.
Akinukuu
Maneno ya kitabu kitakatifu kutoka kitabu cha Nyakati wa Pili 7:18,
Mchungaji Malassy amesema, “Ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu
wataziacha njia zao mbaya wakajinyenyekesha na kuomba nami nitasikia
kutoka mbinguni na nitaiponya nchi yao,” kwahiyo wao kama wakina mama
walioitwa kulia na kuomboleza kwa ajili ya Taifa lao wanayo haki ya
kufunga na kuomboleza kwaajili ya kuliombea Taifa.
Mgeni
Rasmi wa Kongamano hilo anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. Vile vile, viongozi
wanawake kutoka nchi za Afrika ya Kusini, Marekani, Uingereza, Zambia,
Kenya, Kongo na Botswana pia watakuwepo katika kongamano hilo.
Kongamano
hilo limekuwa likifanyika kila mwaka mwezi Disemba na Julai ambapo
hufanyika pamoja na mkesha mkubwa wa maombi katika uwanja wa Taifa,
lengo likiwa ni kuombea amani, utulivu, upendo pamoja na
kuwaombea viongozi wa Serikali ili waongoze Nchi kwa hekima na busara
kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
0 comments:
Post a Comment