Imeandikwa na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Mambo ya Nje wa zamani wa Japan na Mbunge mwakilishi wa
wabunge wa Japan wanaoshughulikia masuala ya Afrika katika Bunge la nchi
hiyo, Ichiro Aisawa amesema ameona tatizo la msongamano wa magari
jijini Dar es Salaam na atazungumza na serikali yake kusaidia kulitatua.
Aisawa alisema hayo jana alipofanya mazungumzo na Rais John Magufuli,
Ikulu, Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Balozi wa Japan
nchini, Masaharu Yoshida. Aidha, Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya
Japan kwa namna inavyoshiriki katika miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo
miundombinu nchini na ameiomba isaidie kujenga barabara za juu au za
chini makao makuu ya nchi, Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa
katika mazungumzo hayo, Aisawa ametembelea miradi inayojengwa nchini na
kampuni za Japan ikiwemo ujenzi wa barabara za juu (Flyover) wa Tazara
na wa kuzalishaji umeme kwa gesi wa Kinyerezi.
Aisawa baada ya kutembelea miradi hiyo, alimhakikishia Rais Magufuli
kuwa kampuni hizo zitafanya kazi nzuri na zitakamilisha kazi kama
ilivyopangwa. Katika ziara hiyo, alijionea changamoto ya foleni za
barabarani katika Jiji la Dar es Salaam.
Kuhusu msongamano huo, Aisawa alisema baada ya kuona changamoto hiyo
ya foleni katika Jiji la Dar es Salaam, amebaini kuwa nchi yake
inahitaji kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha
miundombinu ya jiji hilo na aliahidi kufikisha ujumbe huo kwa Waziri
Mkuu wa Japan, Shinzo Abe ili kuona namna ya kukabiliana nalo.
Aidha, Aisawa alimpongeza Rais Magufuli kwa uongozi mzuri, kupambana
na rushwa na msukumo mkubwa anaoutoa katika maendeleo, juhudi ambazo
zinasaidia kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za kijamii.
Kwa upande wake, Rais Magufuli pamoja na kumshukuru Aisawa kwa kuja
Tanzania na alimhakikishia kuwa Tanzania inatambua mchango mkubwa ambao
Japan inautoa katika maendeleo, na itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano
na ushirikiano wake na Japan katika masuala mbalimbali.
Dk Magufuli aliahidi kuwa serikali itahakikisha uwekezaji wa kampuni
za Japan nchini unalindwa kama itakavyofanya kwa kampuni ya kutengeneza
rangi ya Kansai Plascon ambayo awali ilijulikana kama Sadolin na kampuni
inayozalisha betri za Panasonic nchini, ili uwekezaji huo ulete manufaa
nchini.
“Naomba unifikishie ujumbe kwa Waziri Mkuu, Shinzo Abe kuwa Tanzania
inamshukuru kwa ushirikiano huu mkubwa, tunamkaribisha sana Tanzania na
kwa kuwa serikali yetu imehamia Dodoma tutafurahi sana kama Japan
itaweka alamu ya urafiki wetu kwa kutujengea barabara za Dodoma mjini,
iwe ni flyover au kilometa 20 za barabara, sawa tu,” Rais Magufuli
alimweleza Aisawa.
Aidha, aliishukuru Japan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza
miradi mikubwa ya ujenzi jijini Dar es Salaam ikiwemo upanuzi wa
barabara ya Mwenge – Morocco utakaoiwezesha barabara hiyo kuwa na zaidi
ya njia nane, ujenzi wa barabara ya Tazara, ujenzi wa daraja la Gerezani
njia nne, na barabara ya Bendera Tatu hadi Kamata.
Alimuomba mbunge huyo kwa kuwa ni mmoja wa wabunge wa Japan
wanaoshughulikia masuala ya Afrika, kuwahamasisha wawekezaji na
wafanyabiashara kutoka Japan kuja kuwekeza zaidi nchini.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment