Imeandikwa na Lucy Lyatuu
BODI ya Mikopo ya Elimu kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HELSB)
imesema wanafunzi ambao hawajapangiwa mkopo ni pamoja na waliokuwa na
udahili katika chuo kikuu zaidi ya kimoja nchini na hata waliothibitisha
awali wakitaja chuo watakachokwenda lakini baadaye wakabadilisha.
Imesema jana jijini Dar es Salaam, kundi lingine la waliokosa mikopo
ni pamoja na waliowasilisha maombi yakiwa na dosari kadha wa kadha na
wengine wakiwa na sifa pungufu za uhitaji wa mkopo.
Bodi hiyo imesema hayo huku wanafunzi waliokosa mikopo wakiendelea
kung’ang’ania kwenye ofisi za bodi hiyo, wakishinikiza wasikilizwe shida
zao waendelee na masomo kwani vyuo vimeshafunguliwa.
Katika kusaidia, HELSB imeahidi kufungua dirisha la rufaa ya kupata
mikopo kuanzia Jumatatu ijayo, Novemba 13, mwaka huu ili kuwapa fursa
wanafunzi ambao hawajaridhika kuwasilisha rufaa zao kupitia vyuo
walivyopata udahili, na majina ya watakaofanikiwa kupata mikopo,
yatatolewa Novemba 30, 2017.
Mkurugenzi Mtendaji wa HELSB, Abdul-Razaq Badru alisema hayo jana
wakati akitoa ufafanuzi kuhusu wanafunzi wa elimu ya juu kukosa mikopo
na kusababisha wavamie ofisi za bodi Mwenge tangu juzi.
Badru alisema kwa takwimu za jana (juzi) wanafunzi 200 awali walikuwa
wamethibitisha vyuo ambavyo wamechaguliwa lakini wakaenda vyuo vingine
wakati fedha za mkopo zikiwa zimepelekwa kabla ya vyuo kufunguliwa na
wanafunzi kati ya 400 na 500 walikuwa na sifa pungufu katika kupata
mkopo hiyo.
Kuhusu wasiopata mkopo, Badru alisema wale waliopangiwa vyuo na
wakaenda vyuo vingine, bodi inawasiliana na vyuo ili kufanya usajili wa
wanafunzi haraka na taarifa zao zifikishe HELSB ili ifanye kazi ya
kuwasilishia fedha zao katika vyuo walivyoripoti kabla ya mwisho wa
mwezi huu wa Novemba.
“Wale ambao taarifa zina upungufu na wana sifa za wazi yatima,
walemavu au waliosomeshwa na taasisi, taarifa zao zitapokewa na
kufanyiwa kazi na zitakazokamilika watapangiwa mikopo wiki hii,”
alisema.
Kuhusu dirisha la rufaa, alisema awali lilikuwa likifunguliwa kwa
siku 90 baada ya vyuo kufunguliwa lakini kufuatia suala hilo, Bodi
imeamua kulifungua tena kuanzia wiki ijayo ili kuwapa fursa nyingine
waombaji wote ambao hawajaridhika kuwasilisha rufaa kupitia vyuo
walivyopata udahili wapangiwe.
“Tunatoa mwito kwa uongozi wa vyuo vyote kupokea maombi ya rufaa za
wanafunzi na kuwasilisha kwa Bodi iweze kutoa orodha ya waombaji
waliofanikiwa rufaa zao ifikapo Novemba 30,2017,” alisema.
Kuhusu upangaji wa mikopo kwa mwaka 2017/18 alisema bajeti ya jumla
ya mikopo kwa kipindi hicho ni Sh bilioni 427.54 kwa ajili ya wanafunzi
122,623 na fedha hiyo inajumuisha malipo ya ada za wanafunzi wenye
mikopo pamoja na fedha za chakula na malazi, vitabu, ada na mahitaji ya
vitivo.
Alisema fedha zilizohitajika kwa ajili ya robo ya kwanza ya mwaka
2017/18 ni Sh bilioni 147.06 ambazo tayari bodi imeshapokea kutoka
serikalini ambapo hadi kufikia Novemba 6, 2017 jumla ya wanafunzi 29,578
wa mwaka wa kwanza wamepangiwa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 96.5.
Alisema fedha hizo tayari zimeshatumwa vyuoni ili kuwawezesha kuanza
masomo na fedha za mikopo ya wanafunzi wote wanaoendelea na masomo
zimetumwa vyuoni ili kuwawezesha kuendelea na masomo.
Alisema kati ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza 29,578, yatima ni 937,
wenye mzazi mmoja 5,118, walemavu 486, wenye uwezo mdogo au kipato duni
23,037, wanawake 9,940 na wanaume ni 19,638.
Kuhusu sifa za msingi za kupata mkopo alisema ni uyatima, ulemavu,
walio na kipato duni wakitoka familia zenye kipato duni, na wenye barua
za uthibitisho walisomeshwa kabla ya kujiunga elimu ya juu.CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment