Imeandikwa na Hellen Mlacky
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk AveMaria Semakafu aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa siku tatu uliowashirikisha wadau wa masuala ya watoto kutoka nchi 40 duniani uliolenga kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo ya watoto.
Mkutano huo umeandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Binadamu ya Chuo Kikuu cha Aga Khan na unahusisha washiriki mbalimbali wakiwamo watafiti, wasomi na watunga sera lengo likiwa ni kubadilishana mawazo na kuongeza uelewa juu ya maendeleo ya watoto tangu wakiwa tumboni mwa mama.
Dk Semakafu alisema maendeleo ya watoto ni msingi wa maendeleo endelevu ya nchi yoyote duniani na kwamba mkutano huo utasaidia kuongeza uelewa kwa washiriki kutambua umuhimu wa malezi bora kwa mtoto.
Alisema malezi hayo bora yataangaliwa katika sekta mbalimbali ikiwamo afya, ulinzi, lishe ili kumuwezesha mtoto kukua katika njia sahihi kwa maendeleo ya maisha yake ya baadaye.
“Zaidi ya watoto milioni 250 duniani kote wanashindwa kuendeleza uwezo walio nao ndani yao kutokana na umasikini, lishe duni na mazingira duni tangu wakiwa na umri mdogo,” alisema.
Mapema Mkurugenzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Binadamu, Profesa Kofi Marfo alisema wajibu wa maendeleo ya watoto ni wa kila mtu kwenye jamii, hivyo kila mtu anapaswa kushiriki katika nafasi yake.
“Tuna jukumu la pamoja kujenga nafasi salama kwa watoto wetu kucheza, kupata maji safi na salama, lishe bora, vituo bora vya afya na hospitali kwa ajili ya watoto wetu,” alisema na kuwahimza wadau wote kutafuta mabadiliko ambayo yatafanya uwekezaji wa muda mrefu wa sera, huduma na mipango ambayo itaimarisha misingi ya maendeleo ya binadamu hususani malezi bora ya watoto.CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment