SERIKALI imetangaza kuwa kuanzia sasa haitapokea dawa za misaada
zinazokaribia kumalizika muda wa matumizi pamoja na zile ambazo inazo
kwenye bohari yake.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu alibainisha hayo jana bungeni na kusema sababu ya uamuzi huo ni
kuondokana na kuwa na akiba ya dawa zilizoharibika.
“Dawa nyingi za msaada tumeona tunaletewa zikiwa zinakaribia kuchina
(kuharibika) au ambazo tunazo kwenye bohari yetu. Mfano unakuta umenunua
dawa za malaria halafu msaada unakuja wa dawa hizo hizo, matokeo yake
zinachina na tumeona nyingi zinaishia kuharibika,” alisema Ummy.
Alitoa maelezo hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa
Siha, Dk Godwin Mollel (Chadema) aliyemtaka kuchunguza tatizo kati ya
viwanda vya dawa, Bohari ya Dawa (MSD) na waingizaji wakubwa wa dawa
kwani dawa nyingi huchomwa moto muda wake wa kutumika ukiwa umekaribia
kumalizika.
Waziri Ummy alisema sababu nyingine za dawa nyingi nchini kuharibika
na kuchomwa moto ni kutokana na kuwepo tatizo la maoteo halisi ya dawa
kutopelekwa wizarani wakati wa kuomba dawa.
Hata hivyo, alisema Tanzania ipo chini kwa wastani wa asilimia ya
dawa zinazoharibika bila kutumiwa na kutakiwa kuteketezwa ambayo ni
asilimia 1.8 tu wakati kiwango cha kimataifa ni asilimia tano.
Alisema maduka ya dawa ya serikali yanatakiwa kuanzishwa na
halmashauri. “Halmashauri ikiweka miundombinu sisi tupo tayari kuiambia
MSD kuwakopesha dawa za hadi Sh milioni 50,” alisema.
Katika swali lake la msingi, Mbunge wa Lupembe, Joram Hongole (CCM)
alisema MSD imekuwa ikichelewesha kupeleka dawa kwenye halmashauri
nchini na kusababisha baadhi ya dawa kupelekwa zikikaribia kuisha muda
wake wa matumizi na hivyo kuisababishia gharama halmashauri kwenye
uteketezaji na kuhoji iweje gharama za uteketezaji zibebwe na
halmashauri badala ya MSD.CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment