MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL Group),
Mohammed Dewji(pichani) amepongeza uamuzi wa Rais wa Tanzania, Dk John
Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kufufua viwanda
ambavyo vilikuwa havifanyi kazi.
Dewji ametoa pongezi hizo wakati akizungumza katika mkutano wa siku
mbili wa Global Business Forum 2017 (GBF) kuhusu Viwanda kwa Nchi za
Afrika uliofanyika Dubai, Falme za Kiarabu (UAE). Mfanyabiashara huyo
ambaye anamiliki viwanda 41 alisema uamuzi aliochukua Rais Magufuli ni
mzuri hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea katika uchumi
wa kati.
“Nianze kwa kumpongeza Rais John Pombe Magufuli kwa shabaha yake ya
viwanda, ni nzuri sababu kuna ongezeko la thamani lakini pia watu
wanaweza kupata ajira na pia hizi biashara zitalipa kodi ambazo
zitaisaidia serikali kuwekeza kwenye mambo ya afya na maji na huduma za
jamii. Mimi shabaha yangu kwenye miaka saba au nane ijayo MeTL Group
tunataka tuajiri watu 100,000,” alisema Dewji.
Dewji ambaye kwa mujibu wa jarida la Forbes ni tajiri namba moja
nchini aliongeza kuwa utendaji wa Rais Magufuli ni wa kasi hivyo
anategemea kuwa katika kipindi cha miaka michache ijayo uchumi wa
Tanzania utakuwa umekuwa sana.
“Mimi naona kwa kasi ya Rais kwenye miaka miwili au mitatu ijayo
tutakuwa tumefika mbali sana, uchumi wetu kwa sasa ni asilimia sita au
saba lakini kama tukitaka kuondoa umaskini lazima nchi yetu ukuaji wa
uchumi uanze kukua kwa zaidi ya asilimia 10, mimi nina muamini sana Rais
na shabaha yake kwa hiyo Mungu atutangulie na sisi tupo nyuma yake
tutafika hivi karibuni,” alisema Dewji.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment