TAASISI ya Matibabu ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) sasa itakuwa
na nafasi nzuri zaidi ya kuhudumia majeruhi wake katika hatua za
kibingwa, baada ya kuzinduliwa kwa benki ya damu katika taasisi hiyo.
Benki hiyo ya damu iliyopatikana kwa ufadhili wa Mfuko wa Kuwait kwa
gharama ya Sh milioni 220 sawa na Dola za Kimarekani 100,000,
imezinduliwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu.Kuwapo kwa benki hiyo kutasaidia kuongeza kiwango
cha akiba ya damu katika taasisi hiyo ambayo inahudumia zaidi majeruhi
wa ajali mbalimbali.
Awali damu kwa ajili ya kusaidia kupatikana kwa tiba za majeruhi wa
ajali ilikuwa inapatikana kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
ambayo nayo imekuwa ikizidiwa. Wakati mahitaji halisi ya damu kwa siku
ni uniti 13 hadi 20, lakini uniti zinazopatikana kwa sasa ni kati ya 5
hadi 10 na hivyo kuwapo kwa benki hiyo kutawezesha kuwapo kwa kampeni ya
kuiwezesha benki hiyo kuwa na akiba ya kutosha.
Akizungumza katika uzinduzi wa benki hiyo jana Dar es Salaam, Waziri
Ummy Mwalimu alisema ipo haja kwa Watanzania kujenga tabia ya kuchangia
damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa nchini. Alisema wananchi wengi
wanampigia simu wakimwomba awasaidie ili wagonjwa wao walioko kwenye
hospitali mbalimbali waweze kupatiwa damu. “Tunakushukuru sana Balozi wa
Kuwait kwa msaada mnaotupatia kwani unaisaidia serikali kutatua
changamoto kwenye sekta ya afya lakini pia kupunguza idadi ya wagonjwa
wanaotakiwa kupelekwa kimatibabu nje ya nchi,” alisema.
Alisema kuwapo kwa damu ya kutosha kutawezesha upasuaji mkubwa ambao
kwa kawaida huhitaji damu ya kutosha kuwapo. “Lengo la serikali ni
kuimarisha matibabu ya kibingwa ili Watanzania watibiwe hapahapa nchini
badala ya kutumia gharama kubwa kuwapeleka nje ya nchi,” alieleza Waziri
Ummy. Kwa upande wake Balozi wa Kuwait nchini, Jasem Al Najeem alisema
kwamba Kuwait kupitia taasisi zake za Kiserikali na za Misaada
inajisikia fahari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha
sekta ya afya nchini.
Alisema ataendelea kuuomba Mfuko wa Kuwait wa kuwasaidia wagonjwa
kuendeleza misaada yake kwa benki hiyo ya damu kama sehemu ya kuunga
mkono kampeni ya kuchangia damu. “Maabara hii ina viwango vya kimataifa
na vile vilivyowekwa na Wizara ya Afya ya Tanzania. Kama tulivyosaidia
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa kutengeneza chumba cha upasuaji na
kufunga vifaa vya kisasa vyenye thamani ya Dola za Kimarekani 135,000,
leo hii tunazindua Maabara ya Benki ya Damu yenye thamani ya Dola za
Marekani 100,000,” alisema Balozi wa Kuwait, Jasem Al Najeem.
Baada ya uzinduzi huo, Balozi wa Kuwait alikuwa wa kwanza kuchangia
damu, lakini pia akina mama 40 kutoka Taasisi ijulikanayo kama ‘Wanawake
Kwenye Usukani’ nao walifika kuchangia damu. Mafanikio kwenye Sekta ya
Afya nchini Waziri wa Afya alitumia fursa hiyo ya uzinduzi wa benki ya
damu jana kuelezea baadhi ya mafanikio ambayo Serikali ya Awamu ya Tano
imeyapata kwa kipindi cha miaka miwili tangu iingie madarakani.
Ummy alisema kwa mwaka 2015/2016, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete
ilikuwa inawafanyia upasuaji wagonjwa 30 kwa mwezi, lakini kwa sasa
imeongezewa uwezo na inawafanyia upasuaji wagonjwa 60 kwa mwezi. Pia
rufaa za wagonjwa kupelekwa nchini India kwa matibabu imepungua kutoka
66 mwaka 2015 hadi kufikia wagonjwa 33 kwa sasa baada ya kuimarishwa kwa
Taasisi hiyo ya Moyo.
“Mwaka 2015, wagonjwa 423 walipelekwa nje kwa matibabu ya magonjwa
mbalimbali kama vile moyo, saratani, figo, masikio na mishipa ya fahamu,
lakini mpaka mwezi wa kumi mwaka huu, idadi hiyo imepungua hadi kufikia
wagonjwa 209. “Mwaka 2015, Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU) kilikuwa
na vitanda 21, lakini mpaka leo kuna vitanda 75,” alieleza Waziri Ummy.
Mafanikio mengine aliyoyataja ni uwezo wa kupandikiza vifaa maalumu
kwa wagonjwa wenye matatizo ya kusikia. Alisema ilikuwa inagharimu Sh
milioni 100 kupata huduma hiyo nje ya nchi, lakini kwa sasa inapatikana
hapa nchini kwa Sh milioni 34. Ili kusaidia upatikanaji wa damu na
kuwafanya wananchi kuchangia kwa urahisi, Waziri Ummy alisema kuwa
serikali imeamua kushusha huduma ya uchangiaji damu kwenye ngazi za
mikoa badala ya kutegemea Mpango wa Taifa wa Damu Salama pekee. Alisema
mpaka sasa huduma hiyo inapatikana kwenye mikoa saba na mikoa mingine
mitano itafuata. Aliwataka MOI kuitunza benki hiyo ya damu kwani ni
ukombozi wa Watanzania wote.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment