Mkuu wa kitengo cha Uwezeshaji na Utawala Bora wa Taasisi ya Tafiti
za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Danford Sango akitoa neno la ukaribisho
kwa washiriki wa warsha ya siku tatu ya uwezeshaji wa maandiko bora ya
utoaji ruzuku iliyoandaliwa na ESRF kwa ufadhili wa Taasisi ya Kimataifa
ya Utafiti wa Maendeleo (IDRC) kupitia Taasisi ya Kimataifa ya
Wanazuoni (Think Tank Initiatives-TTI) na kumalizika mwishoni mwa wiki
jijini Dar es Salaam.
Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) imewezesha warsha ya
siku 3 kuwajengea uwezo watafiti wa ndani waweze kuandika andiko bora la
kuombea fedha kwa ajili ya tafiti.
Warsha hiyo iliyofadhiliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa
Maendeleo (International Development Research Centre-IDRC) kupitia
Jukwaa la Wanazuoni Wabobezi (Think Tank Initiatives), ilifanyika makao
makuu ya ESRF, Dar es salaam.
Akizungumza Jijini hapa, Mtalaamu Mwandamizi wa Programu ya Think Tank
Initiatives anayeshughulikia Sera za Uchumi, Dkt. John Okidi kutoka
(IDRC), amesema kwamba watafiti kutoka nchini za Senegali, Tanzania,
Uganda, Ghana na Kenya walikutana kwa siku tatu kujadili na
kubadilishana mawazo namna ya kujenga uwezo katika kuandika maandiko
thabiti ya kuomba fedha kutoka mashirika mbalimbali ya kimataifa.
Alisema kuna umuhimu wa kufanya andiko linaloeleweka ili kuweza
kushawishi watoa ruzuku kutoa fedha za utafiti ili kuharakisha mapinduzi
ya viwanda nchini.
“Watafiti lazima wawe mstari wa mbele katika kushawishi wanasiasa na
viongozi kutegemea zaidi tafiti katika kuleta matokeo chanya kwa
wananchi na kusukuma umuhimu wa kutumia tafiti katika kufanya maamuzi
kwenye ngazi zote za maamuzi,” aliongeza Dkt. Okidi
Alisisitiza umuhimu wa utafiti katika utungwaji wa sera za maendeleo ya
kiuchumi hususani katika kipindi hiki ambacho Tanzania inafanya mageuzi
makubwa ya kuingia kwenye uchumi wa viwanda.
0 comments:
Post a Comment