KATIKA kuhakikisha inarahisisha usafi rishaji wa mizigo na abiria
katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania imeendelea kufungua mipaka
yake kibiashara na nchi jirani kwa kuanzishia vituo vya utoaji huduma
pamoja.
Baada ya vituo kadhaa kufunguliwa, sasa ni zamu ya kufunguliwa kwa
Kituo cha Utoaji Huduma kwa Pamoja kwenye mpaka wa Tanzania na Uganda
cha Mutukula mkoani Kagera. Ingawa matumizi ya kituo hicho yalianza
Agosti, 2015 lakini ufunguzi wake rasmi unatarajiwa kufanywa keshokutwa
Alhamisi na marais, Dk John Magufuli wa Tanzania na mwenzake wa Uganda,
Yoweri Museveni.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Richard Kayombo alisema ujenzi wa kituo hicho
ulifadhiliwa na Kampuni ya Trade Mark East Africa (TMEA) kwa gharama ya
Sh bilioni 7.1. Mbali na kituo hicho, vituo vingine ambavyo tayari
vilishafunguliwa na sasa vinafanya kazi ni Kituo cha Pamoja cha Holili
kilichopo mkoani Kilimanjaro kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya, na Kituo
cha Rusumo kilichopo wenye mpaka wa Tanzania na Rwanda, wakati ujenzi
wa kituo cha Tunduma kwenye mpaka wa Tanzania na Zambia kimeanza
kujengwa.
Kwa mujibu wa Kayombo, lengo la kujengwa kwa vituo hivyo vya pamoja
ni kurahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria miongoni mwa nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Alisema vituo hivyo vinasaidia
kuondoa vikwazo vya kibiashara na kimatembezi kwa kuwa huduma zote
muhimu za kitaasisi kwa nchi husika zinapatikana eneo moja.
“Kwa mfano, gari likitoka Tanzania litakwenda upande wa Uganda ambako
abiria watahudumiwa na kama ni mizigo hivyo hivyo kwa kuwa kila upande
wa nchi kuna Idara zote na Maofisa wote wa nchi zinazohusika kama vile
forodha na uhamiaji, hii inasaidia kuondoa usumbufu kwa wananchi ndani
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Kayombo.
Faida zitokanazo na kukamilika kwa Kituo cha Mutukula ni pamoja na
ukusanyaji wa mapato ya serikali. Kwa mujibu wa TRA, Shirika la Viwango
nchini (TBS) ambao awali hawakuwepo mpakani hapo, wameweza kukusanya Sh
milioni 380.4 kuanzia Mwezi Novemba, 2015, wakati Idara ya Uhamiaji
wamefanikiwa kukusanya Dola za Kimarekani 115,340 (Sh milioni 253.7 za
Tanzania) kwa mwaka 2016/2017 ikilinganishwa na Dola za Marekani 71,150
walizozikusanya mwaka 2015/2016.
Kwa upande wao TRA wamekusanya jumla ya Sh bilioni 27.78 kuanzia
Agosti, 2015 mpaka Juni, 2017 ikilinganishwa na Sh bilioni 18.65 mwaka
2014/2015. Faida nyingine ambazo nchi inazipata kutokana na kuanzishwa
kwa vituo hivyo vya pamoja ni kubadilishana kwa taarifa na takwimu.
Mkurugenzi huyo wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA alisema kuwa
ni rahisi kwa maofisa kubadilishana taarifa kama kuna kasoro yoyote kwa
abiria au takwimu kuhusu jambo fulani na hivyo kudhibiti vitendo vya
udanganyifu. Aidha, vituo hivyo vya mipakani pia vimewasaidia wananchi
kufanya biashara kwa urahisi kwa kuwa wanatumia muda mfupi katika
kukamilisha taratibu za kutoka na kuingia nchi nyingine. Pamoja na faida
hizo, baadhi ya changamoto zinazovikabili vituo hivyo vya mipakani ni
biashara za magendo.
Kayombo alisema kuwa baadhi ya wananchi walio mipakani huvusha mizigo
yao kutoka upande mmoja wa nchi kwenda upande wa pili kimagendo badala
ya kutumia vituo hivyo. Changamoto nyingine ni uwepo wa nyufa kwenye
jengo hilo la Mutukula zilizosababishwa na tetemeko la ardhi, ukosefu wa
eneo la ukaguzi wa mizigo ya abiria na uhaba wa nyumba za watumishi.
Imeelezwa kuwa baadhi ya changamoto hizo zimeanza kutatuliwa na Mamlaka
ya Mapato nchini.
Aidha, Kayombo alisema kuwa mbali na kufadhili ujenzi wa kituo hicho
cha Mutukula, Kampuni ya Trade Mark East Africa pia kimetoa vifaa
mbalimbali kwa matumizi ya kiofisi kama vile kompyuta, mashine za
ukaguzi pamoja na jenereta.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment