UMOJA wa Ulaya (EU) umetoa Euro milioni 50 (takribani Sh bilioni 130)
kwa ajili ya miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayotekelezwa na
Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Makubaliano ya msaada huo yalisainiwa Dar es Salaam jana kati ya EU
ikiwakilishwa na Kamishna wa Maendeleo, Neven Mimica na Serikali ya
Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ikiwakilishwa na Katibu Mkuu
wake, Dotto James. Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Nishati Jadidifu,
Edward Ishengoma aliiwakilisha Wizara ya Nishati.
Akizungumza kabla ya kusaini makubaliano hayo, Katibu Mkuu James
alisema kiasi hicho cha fedha ni sehemu ya awali ya kiasi cha Euro
milioni 180 zilizotolewa kwa ajili ya kuboresha sekta ya nishati na
kufafanua kuwa fedha hizo zitatolewa katika awamu mbalimbali.
Alisema kati ya Euro milioni 180, Euro milioni 90 zitatumika kwa
ajili ya mpango wa kusambaza umeme vijijini kupitia REA na nyingine Euro
milioni 90 zitatumika kwa ajili ya kuboresha sekta ya nishati kupitia
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na REA.
Aliongeza kuwa msaada huo usio na masharti ni moja ya mikakati ya EU
kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John
Magufuli, katika usambazaji wa umeme vijijini.
Aliishukuru EU kwa msaada huo na kusisitiza kuwa serikali itautumia
msaada huo katika kuhakikisha kuwa vijiji vyote Tanzania vinapata umeme
ifikapo mwaka 2020. Awali akielezea mafanikio ya REA, Katibu Mkuu
alisema wakati REA inaanzishwa mwaka 2008, asilimia mbili tu ya vijiji
vyote vilikuwa vinapata umeme, lakini hadi kufikia Desemba, 2016 ni
asilimia 49.3 wananchi waishio vijijini wanapata umeme.
Aliongeza kuwa mwaka 2008, asilimia 10 ya wananchi kitaifa walikuwa
wanapata umeme, lakini hadi kufikia Desemba, 2016, asilimia 67.5
wanapata umeme wa uhakika. “Mafanikio haya ni makubwa na ninaamini
kupitia msaada huu na ongezeko la kasi ya usambazaji wa umeme vijijini,
ifikapo mwaka 2020 vijiji vyote nchini Tanzania vitakuwa na umeme wa
uhakika na kupelekea kwenda kwenye uchumi wa viwanda,” alibainisha
Katibu Mkuu Hazina.
Naye Kamishna wa Maendeleo wa Umoja wa Ulaya, Mimica alisema umoja
huo unatambua juhudi zinazofanywa na serikali kupitia Wizara ya Nishati
katika usambazaji wa umeme vijijini hivyo wapo tayari kuisaidia itimize
malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa yenye lengo la kuhakikisha
Tanzania inakuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Mimica alisema nishati ya umeme ni muhimu hususan katika maeneo ya
vijijini kwa kuwa inachangia uboreshaji wa huduma za jamii kama shule,
vituo vya afya, hospitali, viwanda vidogo vidogo na kilimo. Alisema
kupatikana kwa umeme wa uhakika vijijini kutawezesha ongezeko la ajira
kwa kuwa wananchi watajiajiri kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya
kusindika mazao.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment