SHIRIKA la Umeme nchini (TANESCO) Kanda ya Dar es Salaam na Pwani
limetumia Sh milioni 400 kurudisha katika hali yake, miundombinu ya
umeme iliyoharibiwa na mvua za wiki iliyopita.
Aidha kukatika umeme baadhi ya maeneo kumeisha baada ya kituo cha
kuzalisha umeme kwa gesi asilia cha Kinyerezi I kuanza kufanya kazi
usiku wa kuamkia jana. Hayo yalibainishwa na Meneja Mwandamizi wa
Tanesco Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, Mahende Mugaya alipozungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam. Alikuwa akizungmza katika kikao cha
mameneja wa shirika hilo kanda zote za Dar es Salaam kilichofanyika
katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda.
Alisema mvua zilizonyesha ziliharibu miundombinu mingi ya umeme
katika maeneo hayo na pamoja na kurekebisha miundombinu hiyo, Tanesco
imepoteza mapato ambayo yangepatikana katika maeneo yaliyopata hitilafu
ya umeme. “Hakuna mtu anayeweza kuzuia mvua lakini tunapambana kuboresha
miundombinu yetu hasa katika kipindi hiki ambacho mvua zaidi
zinatarajiwa kunyesha,” alisema Mugaya.
Aidha alisema kukatika kwa umeme katika baadhi ya maeneo kumekwisha
kuanzia leo (jana) kwani mitambo mingi imerekebishwa, ikiwa ni pamoja na
kuvuja kwa gesi eneo la Kinyerezi I hivyo suala la mgawo litakwisha.
Alisema kuelekea mvua zinazotarajiwa kunyesha shirika linahakikisha
uharibifu mkubwa hautatokea kwa kukata miti mikubwa iliyo karibu na
laini za umeme ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikichangia uharibifu
hasa wakati wa mvua. Makonda alisema lengo la kikao hicho ni kujadili
mahitaji ya umeme kwa mkoa, kero ya kukatika umeme mara kwa mara (mgao).
Mengine ni kuangalia mpango mkakati wa kukabiliana na madhara
yatokanayo na mvua zinazoendelea kunyesha na mpango mkakati wa
kuhakikisha taasisi za umma zikiwemo shule, vituo vya Polisi na vituo
vya Afya vinakuwa na umeme wa uhakika. Alisema kukatika kwa umeme mara
kwa mara imekuwa kero kubwa kwa wananchi na wakati mwingine kusababisha
hasara hivyo anaamini Tanesco itamaliza kero hizo.
Aidha Makonda alitoa mwito kwa mameneja na watendaji wengine kuwa na
lugha nzuri kwa wateja wao na kufika kwa wakati pale wanapopata taarifa
za tatizo la umeme ili kuhakikisha hakuna uharibifu unaotokea kwa wateja
tatizo la umeme linapotokea.
“Hakikisheni kauli zinakuwa nzuri mtu anapopewa taarifa na anasema
anakuja ndani ya dakika tatu basi ahakikishe anafika ili watu wasipate
tatizo zaidi,”alisema. Kaimu Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Leila Muhaji
alisema tatizo la kukatika umeme kwa baadhi ya maeneo nchini limeisha
baada ya kituo cha kuzalisha umeme kwa njia ya gesi asilia cha Kinyerezi
I kuanza kazi usiku wa kuamkia jana.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment