Imeandikwa na Hellen Mlacky
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imesema ushirikiano
wa kibiashara kati yake na Zambia umeimarika, ambako mizigo yake
inayopita katika bandari hiyo imeongezeka kutoka tani 1,248,000 kwa
kipindi cha Januari hadi Septemba, 2016 hadi tani 1,478,000 kwa kipindi
kama hicho mwaka huu.
Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa TPA, Lydia Mallya aliyasema hayo jana
jijini Dar es Salaam baada ya kupokea ujumbe wa wafanyabiashara 10
kutoka Zambia ambao wanapitisha mizigo yao katika Bandari ya Dar es
Salaam. “Mizigo hii inapita kwenda nchi za nje na pia wanaingiza kutoka
nchi za nje ikiwemo shaba, mafuta, mahindi, mbolea na ngano na dhumuni
la wao kuja hapa ni kuona jinsi bandari ilivyozidi kuboreshwa na usalama
uliopo,” alisema Mallya.
Alisema bandari hiyo ina usalama wa hali ya juu na kuwahakikishia
wafanyabiashara hao kutoka Zambia kwamba TPA itaendelea kuhudumia mizigo
yao kwa asilimia 100 na watakuwa wanafanya nao kazi kwa karibu ili
kuzidi kuvutia shehena nyingi zaidi inayotoka Zambia. “Bei zetu za
huduma ni shindani ukilinganisha na bei za bandari nyingine kwa hiyo
hatuna hofu, tunawakaribisha kwa mahojiano zaidi na tumewaambia mtu
akiwa na mzigo mkubwa zaidi atapata bei ambayo ni nzuri ili wazidi
kupitisha mizigo yao katika bandari ya Dar es Salaam,” alifafanua.
Aliongeza, “Kwa kweli mzigo wa Zambia ni mkubwa sana unaopita katika
Bandari ya Dar es Salaam, kwa sababu kuna shehena kubwa ya shaba inapita
katika bandari yetu, pia tunapokea mbolea nyingi ambayo inaenda
Zambia... ukiangalia umbali wa hapa na China ni karibu zaidi kuliko
bandari nyingine.”
Alisema baada ya kuzungumza na kujadiliana nao kwa kina,
waliwatembeza na kuwaonesha huduma zinazotolewa na Bandari ya Dar es
Salaam ikiwamo kuangalia mizigo inavyohudumiwa katika Kitengo cha
Makasha, magari, mbolea, mafuta na eneo linalowekwa mizigo kwenye
makontena ili kuisafirisha kupeleka nje ya nchi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu TPA, Lazaro Jacoba alisema
masuala ya usalama kwa bandari zinazosimamiwa na TPA yameimarishwa
ambapo serikali yenyewe imetoa msukumo mkubwa na hivyo kuwekwa mifumo
sahihi ya kuhakikisha usalama wa mizigo ya wateja usio wa wasiwasi.
“Mfano Bandari ya Dar es Salaam ina mfumo wa kiusalama wa kisasa na
sina hakika kama kuna taasisi nyingine nchini ina mfumo huu ambao ni
unganishi wa kitehama ambao unafanya kazi ya ulinzi na kazi ya
utekelezaji wa mizigo uende pamoja,” alisema Jacoba.
Alisema mfumo huo unaiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kuwa na kamera
za usalama (CCTV) zaidi ya 400 na mifumo mingine ya ugunduzi wa
kielektroniki unaofanywa taarifa za matukio zisambae kupitia simu za
mikononi na mifumo mingine ya mawasiliano.
“Changamoto ya wizi inaonekana siyo ya bandari ila ni mizigo ya
barabarani lakini kwa kuwa wateja wamesema baada ya kugundua bandari ni
salama, lakini wateja wanapata changamoto barabarani tuliteua wataalamu
wa usalama wa vyombo vyote vya ulinzi Tanzania ambao kwa maelekezo ya
serikali wapo bandarini,” alieleza.
Alisema wataalamu hao walizunguka kutazama njia zote mpaka kwenye
mipaka ya Tanzania na wateja wao na waligundua mambo kadhaa
yanayosababisha upotevu wa mizigo barabarani, ikiwemo kutumwa
wawakilishi na madereva wasio waaminifu.
“Tumechukua hatua na kwa sasa hali ya barabara hizo ni salama na
mawasiliano ni mazuri na makamanda wa mikoa yote tunashirikiana nao na
pia tunaifuatilia mizigo ikiwa barabarani kwa kutumia mifumo yetu, hivyo
hali ni nzuri na kazi ya kupambana na uhalifu ni endelevu,” aliongeza.
Naye Kaimu Meneja wa Bandari, Ahmad Mchalaganya alisema kuhusu wizi
wa mizigo wamejiimarisha kiulinzi na mizigo inayoenda nje wamefunga
vifaa kwa ajili ya kuangalia mizigo njiani ili kudhibiti wizi.
Mapema, Kiongozi wa ujumbe huo ambaye ni Rais wa Chama cha Biashara
na Viwanda Zambia, Michael Nyirenda alisema wataendelea kushirikiana na
mamlaka hiyo kibiashara, huku akiomba wasafirishaji wa Zambia waruhusiwe
kuingia Tanzania na kufanya biashara.
Aidha, Makamu wa Rais Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA),
Edward Urio aliipongeza TPA kwa kuimarisha usalama bandarini na kufunga
kamera na kuboresha mifumo yao pamoja na kupunguza muda ambao mzigo
unatolewa ndani ya bandari.
Alisema hali hiyo imewavutia zaidi wafanyabiashara wanaoitumia
bandari hiyo wakiwemo kuutoka Zambia kuendelea kufanya kazi na TPA. “Ni
majukumu yetu bandari na wadau kukaa chini na kuangali ni kitu gani
walikuwa wanafaidika katika hizo bandari zingine ili na sisi tuwapatie
huduma bora zaidi ili kuhakikisha mizigo yote inayoingia na kutoka
Zambia inapita katika Bandari ya Dar es Salaam,” alisema Urio.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment