Imeandikwa na Lucy Ngowi
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewataka mabaharia na
manahodha wa meli nchini kushirikiana na serikali kufichua wanaoingiza
mizigo ya magendo na dawa za kulevya kupita ukanda wa bahari.
Makonda alisema hayo jana alipokuwa akifungua warsha ya mafunzo ya
Sheria ya Kazi ya Mwaka 2006 kwa mabaharia jijini Dar es Salaam. Alisema
endapo eneo la bahari litakuwa na wazawa, watatoa taarifa kwa serikali
kuhusu uhalifu unaoendelea huko, hali itakayosaidia kufahamu shughuli
haramu za uvuvi zinazoendelea katika bahari.
“Mabaharia wanaweza kutoa taarifa muhimu kuhusu dawa zinazopitishwa
baharini kwani serikali imekuwa ikishughulika na suala hilo ili
kulidhibiti. Tusaidieni tujiepushe na hatari kubwa inayokabili kizazi
chetu. Pia kwenye mali za magendo ambazo hazilipiwi kodi,” alisema
Makonda.
“Ubaharia ni kazi muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa
kupitia Ukanda wa Bahari, mabaharia wanapaswa kuona wana jukumu la
kuchangia ukuaji wa pato la taifa,” alisema Makonda.
Akisoma risala kwa niaba ya wenzake, Aloyce Mpazi alisema wanakosa
ajira katika meli na kampuni zinazofanya utafiti na uchimbaji wa mafuta
na gesi Mtwara, Tanga na maeneo mengine tofauti na nchi nyingine
zinazotoa kipaumbele cha ajira kwa mabaharia wao.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment