Imeandikwa na Mwandishi Wetu
RAIS John Magufuli ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)
kuvunja sehemu ya Jengo la Makao Makuu ya Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) na la Wizara ya Maji na Umwagiliaji yaliyopo katika hifadhi ya
barabara ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya daraja la ghorofa tatu la
Ubungo (Ubungo Interchange) jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo jana baada ya kukagua maendeleo ya
ujenzi wa daraja la juu la Tazara (Tazara Fly-Over) na Ubungo
Interchange muda mfupi baada ya kurejea Dar es Salaam kutoka kijijini
kwake Chato mkoani Geita.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, akikagua maendeleo ya ujenzi wa
daraja la Ubungo, Rais Magufuli amemuagiza Meneja wa Tanroads Mkoa wa
Dar es Salaam, Ndyamukama Julius kuvunja sehemu ya jengo la Tanesco na
la Wizara ya Maji na Umwagiliaji yaliyopo katika eneo la hifadhi ya
barabara ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya daraja hilo.
“Sheria ya hifadhi ya barabara katika eneo hilo ni mita tisini kila
upande kutoka katikati ya barabara hivyo ni lazima sheria hiyo
iheshimiwe ili kuharakisha ujenzi wa daraja la ghorofa tatu katika eneo
hilo la Ubungo unafanyika bila vikwazo kwani sheria ni msumeno haina
budi kuzingatiwa hata na serikali yenyewe,” alisema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli ameiagiza Tanroads kutangaza zabuni ya ujenzi wa
barabara yenye urefu wa kilometa 16 kutoka eneo linapoishia daraja la
ghorofa tatu katika eneo la Ubungo kwenda Chalinze ili itanuliwe kwa
lengo la kurahisisha usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.
Rais Magufuli amewataka makandarasi wanaojenga daraja la Tazara na
Ubungo kuharakisha ujenzi wa madaraja hayo usiku na mchana ili
yamalizike kwa wakati ama kabla ya muda huo katika kurahisisha maendeleo
ya kibiashara katika Jiji la Dar es Salaam.
“Dar es Salaam ni jiji la kibiashara, hivyo hakuna budi miundombinu
yake ya usafiri iweze kurahisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kutoka
ndani ya jiji na nje ya Jiji la Dar es Salaam,” alisema Rais Magufuli.
Baada ya kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA), Rais Magufuli akiwa ameongozana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alikagua
ujenzi wa Daraja la Juu Tazara (Tazara Fly-Over).
Mhandisi wa Masuala ya Usalama wa Ujenzi, Richard Baruani alimueleza
Rais Magufuli kuwa ujenzi wa Daraja la Tazara umefikia asilimia 64, na
linatarajiwa kukamilika Oktoba mwakani. Kwa upande wa Daraja la ghorofa
tatu la Ubungo, Mhandisi Mshauri Reginald Kayanga alisema ujenzi wake
unatarajiwa kuanza rasmi mwezi ujao.
Machi 20, mwaka huu, Rais Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi
wa barabara za juu Ubungo utakaochukua miezi 30 kuanzia sasa hadi
Septemba 2019. Mradi utagharimu takribani Sh bilioni 188.71 ukiwa na
lengo la kupunguza msongamano wa magari katika barabara za Morogoro,
Nelson Mandela na Sam Nujoma.
Fedha za mradi wa ujenzi wa barabara zenye ghorofa tatu, umefadhiliwa
na Benki ya Dunia ambayo imetoa zaidi ya Sh bilioni 186.7 kwa ajili ya
gharama za usanifu, usimamizi na ujenzi wa mradi wakati serikali
ikichangia zaidi ya Sh bilioni 1 kwa ajili huduma nyingine ikiwemo
ulipaji fidia wa nyumba zitakazoathiriwa na mradi huo.
Alipozindua ujenzi huo, Dk Magufuli aliitaka Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Tanroads kumsimamia mkandarasi Kampuni
ya China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC) kujenga
barabara za viwango pamoja na kukamilisha ujenzi wake haraka.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment