Imeandikwa na Hellen Mlacky
MAMIA ya watu wakiwemo waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali
vya habari jana walishiriki ibada ya kumuaga Rose Athumani (41)
aliyekuwa Mwandishi wa Habari Mwandamizi wa Kampuni ya Magazeti ya
Serikali (TSN) inayochapisha magazeti ya Daily News, HabariLeo na
SpotiLeo.
Rose alifariki dunia usiku wa Novemba 9, mwaka huu katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa kwa
matibabu. Aliagwa jana katika Kanisa Katoliki la MNH na anatarajiwa
kuzikwa leo Kijiji cha Ongoma, Uru Kaskazini, wilayani Moshi mkoani
Kilimanjaro.
Ibada hiyo iliongozwa na Padri Paulo Chiwangu wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania (TEC) na Shemasi Raymond Mukhotya, aliyetoa mwito kwa
jamii kusaidia watu wakiwa hai badala ya kusubiri wakiwa wamefariki
dunia.Mukhotya alisema jamii kwa sasa imekuwa ikijisahau kuwasaidia watu
wenye mahitaji mbalimbali, wakiwemo wagonjwa lakini wamekuwa
wakijitokeza kwa wingi kuwasaidia waliokufa.
“Unaweza ukakutana na mgonjwa anatembea na fomu ya kuomba msaada hadi
inachakaa mkononi mwake hapati msaada, lakini inapotokea amekufa
unaweza kuona mtu anajitokeza hata kununua jeneza peke yake. Mtu akifa
anakuwa mzuri kuchangiwa,” alisema Mukhotya. Aidha, alisema kifo ni
fumbo la juu kabisa kwa wanadamu na hakizoeleki na kwa Mkristo kifo siyo
mwisho, bali ni daraja na safari ya kuelekea nchi ya ahadi.
Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim Yonazi alitoa pole na kuishukuru
familia kwa kuwapatia zawadi ya Rose aliyekuwa rafiki, dada na
mfanyakazi wa TSN aliyefanya kazi yake kwa weledi wa taaluma yake.
“Kumbukumbu yake itabaki katika maisha yetu, nawashukuru wafanyakazi wa
TSN mlivyojitoa na ninawapa mwito tuangalie yale mazuri Rose
aliyotuachia iwe hazina katika maisha yetu na hivyo ndivyo tutakavyoweza
kumuenzi,” alisema Dk Yonazi.
Naye Mhariri wa Habari wa Daily News, Leonard Mwakalebela alisema
Rose alikuwa kipenzi cha kila mtu na alikuwa mchapakazi wa aina yake
katika kipindi chote. “Hata alipoanza kuumwa bado alikuwa anakuja
kazini, alikuwa anaweza kufanya kazi yoyote, hakatai kazi unayompangia,
hachagui kazi, tunasikitika kwa sababu alipenda kazi yake iwe bora ili
inapotoka na jina lake aonekane kweli amefanya kazi, hivyo tumepoteza
kipenzi, tumepoteza kamanda,” alisema.
Akizungumzia utendaji kazi wa Rose, Mwandishi wa Kituo cha
Televisheni cha Channel Ten, Kibwana Dachi alisema wamepoteza mwandishi
mzuri katika tasnia kwa kuwa alikuwa ni mwandishi mzuri aliyebobea hasa
katika habari zake alizokuwa akiziandika na kuchapishwa gazetini.
Ofisa Habari wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Magreth Chambiri alisema
Rose alikuwa mchapakazi na mcheshi na kazi zake zilikuwa ni za kuvutia,
hivyo tasnia ya habari imepoteza mwanahabari mahiri na kutoa mwito kwa
wanahabari wengine kuiga mfano wa Rose.
Mwandishi wa Habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Kuluthum
Ali alisema ingawa hakuwa akifanya kazi ofisi moja na Rose, bado
alikuwa ni rafiki yake wa karibu, hivyo kuondoka kwake ni pigo kubwa kwa
tasnia ya habari, jamii na mtoto wake ambao wote walikuwa wakimtegemea.
Naye Mjomba wa marehemu, Cornelius Kariwa alisema Rose alizaliwa
Septemba 22, 1976 Moshi mkoani Kilimanjaro.
Ameacha mtoto wa kiume, Michael Edward (Brian). “Rose alikuwa mtoto
mwema mwenye karama nyingi na tulimkumbatia, alikuwa na bidii nyingi ya
kujiendeleza. Tunawashukuru wote walioshirikiana nasi tangu alipougua na
katika ibada hii wakiwemo wafanyakazi wenzake,” alisema Kariwa. Rose
amepata elimu hadi ngazi ya Chuo Kikuu na aliajiriwa rasmi na TSN mwaka
2009. Hadi mauti yanamkuta, alikuwa akifanya kazi ya Mwandishi wa Habari
Mwandamizi na Makala katika gazeti la kila siku la Kiingereza la Daily
News.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment