Imeandikwa na Mwandishi Wetu
WANAHISA wa Kampuni ya Uwekezaji ya TCCIA wamekubaliana kuwekeza
zaidi kwenye miradi mikubwa ikiwemo kujenga maghala ya kuhifadhia mazao
na nyumba za biashara katika miji inayokua kwa kasi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye Mkutano Mkuu wa 12 wa Mwaka
wa Wanahisa, wajumbe wa mkutano huo uliofanyika Dar es Salaam mwishoni
mwa wiki, walisema wameridhishwa na maendeleo na uendeshaji wa kampuni
hiyo.
“Kazi iliyofanyika ni kubwa na inaonekana wazi, tunawapongeza
viongozi wetu na waasisi wa wazo hili lililozaa kampuni ya Uwekezaji ya
TCCIA ambayo sasa ina wanahisa wengi waliowekeza kiasi kikubwa cha
fedha,” alisema Mokoro Maguye kutoka Serengeti.
Akizungumza baada ya mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi,
Aloys Mwamanga alisema ajenda ngumu ilikuwa kupunguza idadi ya wajumbe
wa bodi kutoka 11 hadi kufikia saba ili kupunguza gharama za kampuni.
“Yapo masuala mengine kama uwekezaji kwenye majengo na maghala, hili
limepitishwa na tayari tumeshapata viwanja mkoani Mtwara kwa ajili ya
kujenga maghala ya kuhifadhia mazao,” alisema.
Awali akitoa elimu kuhusu masuala ya hisa, Mjumbe wa Bodi ya kampuni
hiyo, Alphaxad Masambu, alisema, “Taifa lolote unaloona limeendelea ujue
lina soko la hisa, masoko ya hisa katika mataifa makubwa yana umaarufu
mkubwa katika vyombo vya habari kwa sababu asilimia kubwa ya wananchi
wake wamenunua hisa katika kampuni mbalimbali.”
Kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 2005 kwa kununua hisa za NMB, na hadi
sasa uwekezaji wao una thamani ya Sh bilioni 28, wanatazamia kuwekeza
kwenye ujenzi wa maghala mkoani Mtwara, nyumba za biashara Dodoma, Dar
es Salaam na Tanga ambapo hadi sasa uchambuzi yakinifu wa miradi hiyo
unaendelea.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment