Imeandikwa na Mwandishi Wetu
ALIYEKUWA Mhasibu Mkuu wa Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), Godfrey Gugai amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu akituhumiwa kuwa na mali zenye thamani ya zaidi ya
Sh bilioni 3.6 kinyume na kipato chake.
Gugai amepandishwa kizimbani katika mahakama hiyo sambamba na
washitakiwa wengine watatu ambao ni George Makaranga, Leonard Aloys na
Yasini Katera ambao kwa pamoja wanakabiliwa na makosa 42 yakiwamo ya
kugushi mikataba ya mauzo ya viwanja vilivyoko maeneo mbalimbali nchini
na utakatishaji wa fedha.
Mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi, Thomas Simba, washitakiwa wote wamekana
kutenda makosa hayo. Hakimu aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 4,
atakapotoa uamuzi juu ya pingamizi lililowasilishwa na upande wa utetezi
kuhusu uhalali wa makosa ya utakatishaji fedha.
Washtakiwa wote walipelekwa rumande kusubiri siku ya shauri hilo.
Upande wa Mwendesha Mashitaka ukiongozwa na Mwanasheria wa Serikali,
Wankyo Simon na mawakili kutoka Takukuru, Vitalis Peter na Max Ally,
uliitaarifu Mahakama hiyo kuwa uchunguzi wa shauri hilo bado
haujakamilika.
Kabla ya kesi hiyo kupangiwa tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,
wakili anayewatetea washitakiwa, Alex Mgongolwa aliiomba mahakama ifute
mashitaka 21 yanayohusiana na utakatishaji wa fedha kwa kuwa taarifa
zilizowasilishwa mahakamani hapo hazioneshi vionjo vinavyounda mashitaka
yaliyoainishwa kwa mujibu wa sheria.
Mgongolwa aliiambia Mahakama kuwa utakatishaji fedha siyo kosa la
msingi, lakini ni kosa la pili ambalo mtu hawezi kushitakiwa kama
upelelezi wa shitaka la msingi haujakamilika.
Alidai kama mtuhumiwa akishitakiwa kwa kosa hilo la pili, upande wa
mashitaka unapaswa kuonesha vionjo vyote vinne vinavyounda kosa hilo la
kutakatisha fedha. Wakili huyo alidai kuwa, kwa kusoma mashitaka
yaliyoainishwa mbele ya washitakiwa bila vionjo vyovyote
vilivyobainishwa, na kwa msingi huo mashitaka ya aina hiyo hayawezi
kusimama kwa vile hayamwezeshi mshitakiwa kujua msingi wa mashitaka yake
ili aweze kujitetea.
Hata hivyo, upande wa mashitaka uliiomba Mahakama kutupilia mbali
pingamizi la utetezi ukidai halina msingi kisheria. Wakili Wankyo Simoni
alibainisha kuwa, hati ya mashitaka ilipokelewa na kusajiliwa na
Mahakama kabla ya kusomwa mbele ya washitakiwa.
Aliiambia mahakama kuwa vionjo vyote vinavyounda kosa la utakatishaji
fedha vimeanishwa na ndiyo maana washitakiwa waliweza kuelewa
waliposomewa na kukana kuhusika.
Alidai kama kuna dosari katika mashitaka hayo, mahakama inaweza
kufanya marekebisho katika hati ya mashitaka na siyo kuyafuta kama
inavyodaiwa na upande wa mashitaka.
Akisoma mashitaka, mwendesha mashitaka aliiambia Mahakama kuwa kati
ya Januari mwaka 2005 na Desemba mwaka 2015 jijini Dar es Salaam, akiwa
mtumishi wa umma na mwajiriwa wa Takukuru, Gugai alikutwa anamiliki mali
mbalimbali zenye thamani ya Sh billioni 3.6 ambazo haziendani na kipato
chake cha Sh millioni 852.2 kwa muda wote alipokuwa kazini.
Upande wa mashitaka ulidai kuwa alipotakiwa kueleza namna alivyopata
mali hizo, mtuhumiwa huyo alishindwa kutoa maelezo ya kujitosheleza.
Mahakama ilielezwa pia kuwa, kati ya Januari na Juni 2016 jijini Dar es
Salaam, kwa nia ovu, Gugai alighushi mikataba 14 ya mauzo ya viwanja
mbalimbali.
Kwa mujibu wa upande wa mashitaka, mshitakiwa alidanganya kuwa
viwanja hivyo aliviuza kwa nyakati tofauti tofauti kwa Zena Mgallah,
Saleh Asas, Arif Premji, Edith Mbatia, Manwal Masalakulangwa, Rose
Abdallah na Patrick Magesa, madai ambayo siyo sahihi.
Upande wa mashitaka umebainisha kuwa, viwanja hivyo vipo katika
maeneo ya Gomba (Arumeru-Arusha), Mbweni JKT, Ununio (Kinondoni-Dar),
Mwambani na Mwakidila Magaoni, Mwarongo Tanga, Bunju, Kaole Bagamoyo,
Buyuni Temeke, Be-Centre na Itega Dodoma na Nyegezi Mwanza.
Imedaiwa pia kuwa, katika kipindi hicho hicho, Gugai na Makaranga
walighushi hati moja ya mauzo ya kiwanja kilichopo Bunju katika Manispaa
ya Kinondoni akidai kuwa kiliuzwa kwa Makaranga, kitendo ambacho siyo
kweli.
Upande wa mashitaka ulidai kuwa Gugai na Aloys walighushi mikataba
minne ya mauzo ya viwanja vilivyopo maeneo ya Nyamhongolo, Bugarika,
Biseke na Nyegezi jijini Mwanza, akidai kuwa Gugai aliviuza kwa Aloys
wakati ni uongo.
Mahakama ilielezwa pia kuwa kati ya Januari na Juni 2016 jijini Dar
es Salaam, Gugai na Katera walighushi mikataba miwili ya mauzo ya
viwanja vilivyopo Nyegezi Mwanza akionesha kuwa Gugai ameviuza kwa
Katera, madai ambayo siyo ya kweli.
Upande wa mashitaka umebainisha kuwa katika kutenda makosa ya
utakatishaji fedha, Gugai na washitakiwa wengine kwa namna tofauti
walichepusha umiliki halisi wa viwanja hivyo kwa kudai kuwa vilikuwa
vimenunuliwa na watu mbalimbali.
Aidha, upande wa mashitaka ulidai kuwa Gugai na washitakiwa wengine
walijua kuwa viwanja hivyo vilikuwa ni zao la uhalifu wa kosa la rushwa
ambalo nikukutwa na mali isiyoelezeka namna iliyopatikana kwa
kulinganisha na kipato halisi cha mshitakiwa.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment