Jengo la Tanesco |
Juzi Rais Magufuli aliwaagiza Tanroads kuvunja sehemu ya majengo hayo
yaliyopo katika hifadhi ya barabara ili kupisha ujenzi huo unaotarajiwa
kugharimu zaidi ya Sh bilioni 188.71 hadi kukamilika kwake Septemba,
2019.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Ndyamukama alisema
wameanza kutoa notisi jana ili kuwapa muda wamiliki hao kuhamisha mali
zao. Alisema majengo hayo yote yapo katika hifadhi ya barabara na
yanatakiwa kuondoka, ila Rais alisema kama ikishindikana waondoe sehemu
ya majengo hayo.
“Zoezi la ubomoaji huwa lina utaratibu wake ni lazima tuwape notisi,
hivyo tumewapa notisi ya mwezi mmoja ili waanze kuhamisha mali zao na
kubomoa wakishindwa baada ya hapo sisi ndiyo tutabomoa,” alieleza
Ndyamukama.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano- Ujenzi, Joseph Nyamhanga alisema watatekeleza kwa haraka
maagizo hayo ili mradi huo ukamilike kwa wakati na kwa muda uliopangwa
na kuondoa changamoto ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es
Salaam.
Mradi huo ni kati ya miradi mikubwa inayotekelezwa ikiwa ndani ya
Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2015- 2020
waliyoiahidi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015 na umelenga
kupunguza msongamano wa magari katika barabara za Morogoro, Nelson
Mandela na Sam Nujoma.
Nyamhanga alisema zaidi ya magari 65,000 yanapita kila siku katika
makutano ya barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma eneo la Ubungo
hali inayosababisha msongamano katika barabara ya Morogoro ambayo ndiyo
lango kuu la kuingia na kutoka jijini Dar es Salaam.
“Sisi tumepokea maagizo hayo na kinachotakiwa ni utekelezaji, kwa
hiyo Tanesco na Wizara ya Maji watapewa notisi ili waweze kujiandaa
kuvunja jengo hilo kwa muda unaotakiwa na kama watashindwa tutalivunja
sisi wenyewe,” alifafanua.
Alisema kwa kawaida mtu ambaye ameingia katika hifadhi ya barabara
hutakiwa kuvunja mwenyewe ila anaposhindwa au kuchelewa kufanya hivyo
wanamsaidia kuvunja na yeye kutakiwa kulipa gharama.
Aidha, aliwataka watu wote waliojenga kwenye hifadhi ya barabara nchi
nzima kuondoa nyumba zao na maendelezo hayo kutoka kwenye hifadhi ya
barabara vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment