Imeandikwa na Sophia Mwambe
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) wakishirikiana na wataalamu kutoka
Hospitali ya BLK ya New Delhi, India kwa mara ya kwanza wamefanikiwa
kufanya upasuaji wa kihistoria wa upandikizwaji wa figo.
Upasuaji huo wa kwanza ulifanyika Novemba 21, mwaka huu kwa mwanamke
mwenye umri wa miaka 29 ambaye amepatiwa figo na ndugu yake na alikuwa
katika hatua ya tano ya ugonjwa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema,
upasuaji huo wa kihistoria ni kielelezo cha juhudi za serikali ya Awamu
ya Tano za kuboresha huduma za afya nchini zikiwemo zile za ubingwa wa
daraja la juu.
“Upasuaji huu ni juhudi zinazofanywa na serikali za kupunguza rufaa
za wagonjwa wanaohitaji huduma hizo nje ya nchi na hivyo itaokoa fedha
ambazo zingelipwa nje ya nchi kugharamia matibabu hayo na badala yake
fedha hizo zitatumika katika maendeleo katika maeneo mengine,” alisema
Mwalimu.
Alisema kwa zaidi ya mwaka mmoja hospitali hiyo ilijikita katika
kuwekeza katika kuongeza ujuzi wa wataalamu wa aina mbalimbali wakiwemo
wataalamu wa upasuaji wa kupandikiza figo ambapo wataalamu 19
walipelekwa nchini India kwa mafunzo ya vitendo na wataalamu wawili
walipelekwa nchini Norway.
“Utolewaji wa huduma hii hapa nchini utawezesha kwa kiwango kikubwa
kupunguza gharama kwa serikali kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwakuwa
inakadiriwa kwamba utayarishaji wa mgonjwa kwa ajili ya matibabu ya
upandikizaji wa figo ikiwemo vipimo mbalimbali kwa mpokeaji na mtoaji
pamoja na upasuaji utagharimu wastani wa Sh milioni 21 hii ni nafuu sana
ukilinganisha na gharama ya Sh milioni 80 mpaka 100 iliyokuwa ikitumiwa
na serikali kupeleka mgonjwa mmoja nje ya nchi na kwa mwaka ilikuwa
ikipeleka wagonjwa 35,” aliongeza.
Alisema kutokana na ongezeko la wagonjwa figo nchini serikali
imeanzisha vituo vya utakasishaji damu katika Hospitali za Bugando,
Hospitali ya Rufaa Mbeya, Chuo kikuu cha Dodoma na KCMC kwa hospitali za
serikali pia kwa hospitali za binafsi huduma hiyo inatolewa na
hospitali ya Kairuki, TMJ, Regency, Agha Khan, Access na Hindu Mandal.
Aidha alisema ili kuhakikisha huduma za upandikizaji wa viungo
unaboreshwa wizara yake inaandaa sheria itakayosimamia upandikizaji wa
viungo kwa ujumla. “Hapa tumeandaa tu kanuni ili kuwawezesha Muhimbili
kufanya huduma hii, lakini sasa tunatengeneza sheria itakayosimamia
upandikazi wa viungo kwa ujumla na tulikuwa tunafikiria hata ile ya
upandikizaji wa mtoto na tayari nimeshamuagiza Katibu mkuu kuanza
mchakato huo,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Mtendaji wa MNH, Profesa
Lawrence Museru alisema hospitali hiyo kwa sasa ina wagonjwa wa figo 200
ambao wanapata huduma ya kutakatisha damu.
Alisema asilimia 60 ya wagonjwa hao wanahitaji huduma ya upandikizaji
wa figo pamoja na usafishaji wa damu hivyo kuanza kwa huduma hii
utawezesha wagonjwa kupata huduma hiyo.
“Tunawashukuru sana wenzetu wa BLK kwa kuwezesha huduma hii na leo
tumeandika historia Muhimbili na taifa baada ya kuanza kwa upandikizwaji
huu ni kitu kikubwa cha kujivunia kwa nchi yetu,” alisema Museru.
Naye Kiongozi wa jopo la madaktari hao kutoka BLK, Dk Sunil Prakash
alisema upasuaji huo ni tukio muhimu kwa nchi ya Tanzania ambapo
alishauri wizara ya afya kuhakikisha inatunga sheria kuhusu mambo ya
upandikizaji wa viungo mbalimbali vitakavyopatikana kutoka kwa watu
waliokufa ambavyo vitawekwa kwa watu wenye uhitaji.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment