Serikali
imezindua mkakati unaolenga kutokomeza uvuvi haramu kwa kuanzisha
operesheni ya kutumia ndege maalumu itakayofanya doria katika eneo la
bahari kuu.
Akizungumza wakati wa kuzindua safari ya ndege ya kutoka nchini
Mauritius iliyotua hapa nchini, kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kufanya
doria ya majini, Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Abdallah
Ulega alisema lengo ni kudhibiti uvuvi haramu katika eneo la bahari kuu.
Alisema Serikali ya awamu ya tano imejipambanua juu ya ulinzi wa
rasilimali za nchi, ikiwamo meli ya uhakika ya majini, licha ya kukumbwa
na dhoruba kubwa.
Amesema kutokana na hali hiyo ndiyo maana wameunganisha nguvu kwa pamoja
kati yao na Ukanda wa nchi za Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi
kudhibiti uvuvi haramu kwa njia zote.
“Tunaruhusu ndege ya doria leo, ili kuongezea nguvu njia za kudhibiti
wavuvi haramu, tulianza kwa njia ya bahari na sasa ni kwa njia ya anga.
“Changamoto ya uvuvi haramu ni kubwa, mtu anapiga bomu kwenye matumbawe
anafanya uharibifu ambao kuyatengeneza tena yanachukua zaidi ya miaka
100, huku yeye akiharibu kwa dakika tano, ” alisema Ulega.
Ulega alisema uharibifu huo ndiyo unachangia kuwatia umasikini wavuvi
wengi kwa sababu siyo rahisi kupata samaki karibuni na kulazimika kwenda
mbali ambako siyo rahisi kufika bila kuwa na vyombo maalumu.
Kwa upande wa Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar Hamad Rashid alisema atashauriana na marais wa
pande zote mbili kuangalia namna ya kurudisha Shirika la Uvuvi Tanzania
(Tafico) na Shirika la Uvuvi Zanzibar (Zafico).
Alisema mashirika hayo yakifanya kazi kwa kushirikiana wananchi watapata
fursa ya kufurahia matunda yatokanayo na utajiri uliomo baharini.
“Katika mwendelezo wa kupambana na uvuvi haramu na kulinda bahari ya
Hindi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilifanya mazungumzo ya kuingia ubia
na Serikali ya China na tayari kuna meli 10 zinafanya doria.
“Serikali pia imeagiza boti 500 watakazopewa wavuvi ili wazitumie kuvua
kisasa, pia inasimamia ujenzi wa soko la samaki la kisasa na namna bora
ya kuhifadhi samaki awe katika hali yake ile ile hadi anamfikia mlaji, ”
alisema Rashid.
Alisema uvuvi haramu siyo tu janga kwa kuondoa rasilimali za bahari, pia
ukiachwa uendelee unaweza kuwa chanzo cha biashara nyingine haramu
ikiwamo usafirishaji wa watu, biashara ya dawa za kulevya na
utakatishaji fedha.
Nae Katibu mkuu Uvuvi Dk Yohana Budeba alisema ndege hiyo itafanya doria ya anga kwa siku nne.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya kusimamia uvuvi wa
bahari kuu Hosea Mbilinyi alisema ndege hiyo licha ya kuzunguka angani
ikifanya doria, ina uwezo wa kupiga picha na kueleza kinachoendelea.
Alisema doria hiyo ni ya kikanda ambayo inahusisha nchi nane zikiwamo
Tanzania Kenya, Msumbiji, Ushelisheli, Reunion, Comoro, Mauritius na
Madagascar.
Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya operesheni ya kutumia ndege
maalumu itakayofanya doria katika eneo la bahari kuu kudhibiti uvuvi
haramu, leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Waziri wa Kilimo, Maliasili,
Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid Mohamed.
Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega akishuka kwenye
ndege maalumu itakayofanya doria katika eneo la bahari kuu kudhibiti
uvuvi haramu mara baada ya kuikagua ndani.
Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid
Mohamed na Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega
pamoja na viongozi mbalimbali wakiangalia ndege maalumu ya doria katika
eneo la bahari kuu kudhibiti uvuvi haramu.
Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid
Mohamed naNaibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega na
viongozi mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja
Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega na Waziri wa
Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid Mohamed
akitoa zawadi kwa marubani wa ndege hiyo. Picha zote na Emmanuel
Massaka,Globu yajamii.
0 comments:
Post a Comment