Imeandikwa na Mwandishi Wetu
TARATIBU za mazishi ya Mwandishi wa Habari wa Kampuni ya Magazeti ya
Serikali (TSN), Rose Athuman aliyefariki dunia usiku wa kuamkia jana
kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, zinaendelea nyumbani kwa mjomba
wake Paul Mushi huko Mbezi, Mpigi Magohe jijini Dar es Salaam.
Familia hiyo ilisema Rose alikuwa akisumbuliwa na homa kali
iliyosababisha kifo chake kwenye Hospitali ya Muhimbili alikokuwa
amelazwa. Kwa mujibu wa mjomba wa Rose, shughuli za kuaga mwili
zitafanyika Jumapili na marehemu atasafirishwa kwao Moshi mkoani
Kilimanjaro kwa maziko siku ya Jumatatu.
Ameacha mtoto mmoja wa kiume ambaye yuko kidato cha tatu. Aidha,
waandishi wa TSN wamesema kuwa kifo cha mwandishi mwenzao kimeacha pengo
miongoni mwa waandishi kutokana na weledi aliokuwa nao katika kazi.
Mwandishi wa habari za michezo wa magazeti ya HabariLeo na SpotiLeo,
Rahel Pallangyo alisema kuwa amemfahamu Rose tangu mwaka 2014 na alikuwa
mwandishi makini miongoni mwa waandishi wanawake nchini.
“Kwa kweli ni pigo kubwa sana kwangu. Rose alikuwa ni mtu wa watu na
rafiki wa kila mtu, lakini kubwa zaidi alipenda sana kazi yake. Hakika
TSN imepoteza siyo tu mwanafamilia, bali imepoteza mfanyakazi bora.
Nitamkumbuka kwa ucheshi wake na urafiki wake kwangu,” alisema
mwandishi wa gazeti la HabariLeo, Halima Mlacha. Mlacha alisema
alifahamiana na Rose tangu mwaka 2003 wakiwa Chuo Kikuu cha Uandishi wa
Habari cha Dar es Salaam (SJMC) wakati huo TSJ.
Alisema wakati huo, Rose alikuwa mwaka wa tatu na yeye alikuwa ngazi
ya cheti. Alisema baada ya kuachana na Rose chuoni, wakaja kukutana tena
kwenye kazi ya uandishi wa habari wakati huo Rose akiwa akifanya kazi
na Kampuni ya Magazeti ya Mwananchi upande wa gazeti la The Citizen,
kabla ya kuja kujiunga na TSN na kuandikia gazeti la Kiingereza la Daily
News.
“Rose alikuwa mwandishi makini. Nilimfahamu tangu Desemba, 2016.
Nilipokuja hapa TSN nilianza kutumia kompyuta yake kwa kuwa yeye
mwenyewe alikuwa amesafiri kikazi,” alieleza Mhariri Msanifu wa
HabariLeo, Geofrey Lutego.
Naye Kaimu Mhariri wa Michezo, Zena Chande alisema kuwa alimfahamu
Rose tangu mwaka 2009 alipotokea gazeti la The Citizen. Alisema kuwa
Rose alikuwa ni rafiki wa kila mtu na alikuwa na tabasamu muda wote.
Wasifu wa Rose Alizaliwa Septemba 21, 1976 Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Mwaka 1988-1991 alihitimu masomo yake ya sekondari kwenye Shule ya
Sekondari ya Wasichana ya Matuga iliyopo Mombasa nchini Kenya.
Mwaka 2000-2003 alihitimu Diploma ya Juu ya Uandishi wa Habari kwenye
Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam. Mwezi Julai, 2008 alihitimu mafunzo ya Wataalamu wa
Kimataifa wa Uandishi wa Habari kwenye Chuo Kikuu cha Maine, Marekani.
Julai 2002 alifanya mafunzo kwa vitendo kwa miezi minne kwenye gazeti
la Majira. Agosti, 2002 hadi Julai, 2004 alifanya kazi Radio Tanzania
Dar es Salaam (RTD) kama mwandishi wakati akiwa bado anasoma na baada ya
kuhitimu masomo.
Agosti, 2004 hadi Mei, 2009 alifanya kazi na Kampuni ya magazeti ya
Mwananchi kama Mwandishi wa habari, Mwandishi wa ripoti maalumu, makala
na mratibu wa jarida la elimu.
Kuanzia Agosti, 2009 mpaka mauti yanamkuta, alikuwa akifanya kazi na
Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kama Mwandishi wa habari na makala
kwa gazeti la Kiingereza la Daily News.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment