Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kuku wakiendelea kuandaliwa ndani ya Soko la Kisutu. Picha zote na MaendeleoVijijini.
Na Daniel Mbega,
MaendeleoVijijini
SAUTI za kuku zinasikika hata ukiwa nje ya jengo dogo ndani
ya Soko la Kisutu jijini Dar es Salaam, lakini ghafla zinakoma na zinasikika
nyingine.
Siyo kwamba kuku hao wanahitaji chakula ama wanacheza, bali
hapa ni machinjio, na sauti zinapokoma ujue tayari zimekwishapigwa kisu na
zinaandaliwa kwa ajili ya kitoweo.
Nje ya jengo hilo unaweza kuwa umekuta akinamama wengi
wakiwa wamelundikana huku wakiwa wamekalia ndoo zao.
Hawa nao wanasubiri huduma, wanataka kununua utumbo, miguu
pamoja na vipapatio vya kuku hao wanaochinjwa ili wakafanye biashara.
Akinamama hawa wanatoka katika maeneo mbalimbali ya Jiji la
Dar es Salaam na hapa Kisutu ndiko mahali pekee ambako wanaweza kupata bidhaa
hiyo wanayokwenda kuuza mitaani.
Bila shaka baadhi yetu tumekutana ama tumewakuta akinamama
wakiuza firigisi na utumbo mitaani, basi amini kwamba asilimia kubwa wanapata
bidhaa hiyo katika eneo hili la Kisutu.
Ukiingia ndani ya jengo hilo usishangae ukasalimia
usiitikiwe na watu wengi, japokuwa waliomo ni wengi.
Kabla hujajua usimame wapi, utasikia sauti ya mtu akikutaka
radhi kwamba anaomba kupita ama anataka kuweka mzigo.
Naam. Kila mtu hapa yuko ‘busy’ na kazi inakwenda mtindo
mmoja, na hata kutokukuitikia si kwamba wanafanya kiburi ama hawajakuona, la
hasha. Kwa sababu wanataka kuhakikisha kazi wanayoifanya inakuwa katika hali
bora hasa ikizingatiwa kwamba hicho ni chakula kwa afya ya binadamu.
Mazingira ya ndani yanaridhisha kutokana na usafi ambao
unazingatiwa sana na wahusika licha ya changamoto za hapa na pale.
Hawa ni wanaushirika wa Kisutu Poultry Farm Cooperative
Society (KIPOCOSO), ambao wamekuwepo katika soko hilo kwa zaidi ya miaka 28 na
ndio waanzilishi wa kuchinja kuku jijini Dar es Salaam.
Japokuwa hivi sasa baadhi ya masoko yana machinjio ya kuku,
lakini wengi wanaohusika na uchinjaji wamejifunza ama wamewahi kufanya shughuli
hizo katika Soko la Kisutu.
Kuku walionyonyolewa, kuchunwa ngozi au kukatwakatwa wanaweza
kukutoa udenda wangali wabichi na wamewekwa mafungu mafungu.
“Kila fungu unaloliona hapo lina mwenyewe, hawachanganyani
kabisa,” ndivyo anavyoeleza Bw. Hamisi Malamla, Mwenyekiti wa KIPOCOSO.
Anaongeza: “Kazi yetu hapa ni kuchinja, kuku wote wana
wenyewe na kila mmoja hapa ndani anakwenda hapo nje kwenye mabanda wanakonunua
kuku na kutafuta oda, akiipata anakuja kuchinja na kuwatengeneza.”
Bw. Malamla anasema kwamba, asilimia kubwa ya kuku wanaoliwa
jijini Dar es Salaam wanachinjwa na kuandaliwa katika soko hilo, sehemu ambayo
pia ni maarufu kwa wauzaji wa kuku – wa nyama wa kisasa pamoja na wa kienyeji.
Ndani ya jengo hilo lililowekwa terazo, kujengwa masinki
bora pamoja na majiko matatu makubwa yanayotumia gesi, takriban kuku 3,000
huchinjwa kila siku.
Licha ya kufanya shughuli zao kwa ufanisi, lakini
unapozungumza na wanaushirika hawa utagundua kwamba wana mawazo makubwa ya
maendeleo tofauti na unavyoweza kuwadhania.
“Malengo yetu ni kujikita katika uwekezaji wa kilimo na
mifugo, tunataka tuanze kufuga wenyewe kuku (wa kisasa na kienyeji), kuuza kuku
wenyewe, kutotolesha vifaranga, kutengeneza vyakula vya kuku pamoja na
kusambaza madawa,” anasema Bw. Malamla.
Anasema kwamba, ikiwa wataanza uwekezaji wa kufuga kuku
itakuwa ni hatua kubwa kwao kwani watakuwa na uhakika wa kuchinja na kuuza, na
kwamba oda wanazozipata kwa sasa zitakuwa ni nyongeza tu na ziada.
Malamla anasema, kwa uzoefu walionao, ikiwa watajikita pia
katika ufugaji wanaweza kulisha wananchi wengi jijini Dar es Salaam na kwamba
hata kuku watakaowafuga wanaweza kuongezeka ubora tofauti na baadhi ya wanaouzwa
sokoni hapo ambao mara nyingi huwa hawana uzito mkubwa.
“Tukianza ufugaji ni dhahiri tutaongeza ubora kulingana na
mahitaji ya soko na hatuwezi kubahatisha, kwa sababu hapa wakati mwingine kuku
wanaadimika na inapotokea hivyo maana yake tunakosa kazi ya kufanya,” anasema.
Anaongeza kwamba, tangu uongozi wake ulipoingia madarakani
mwezi Machi 2017 (miezi nane iliyopita) wamefanikiwa kujiwekea akiba ya kutosha
ambayo inawapa msukumo wa kuangalia fursa za uwekezaji ili kuongeza kipato
pamoja na kupanua wigo wa ajira.
Usajili
Mwenyekiti wa Ushirika wa Wachinja Kuku Soko la Kisutu (KIPOCOSO), Bw. Hamisi Malamla (kushoto) akiwa na Mjumbe wa Kamati ya Uongozi, Mzee Shaaban Hassan Bogoma leo hii walipotembelewa na MaendeleoVijijini.
KIPOCOSO, ambacho ni miongoni mwa vikundi nane vinavyounda
Umoja wa Wafanyabiashara Soko la Kisutu (UWASOKI), kilisajiliwa Juni 28, 1989 kama
chama cha ushirika na kupewa hatia namba DSR-382.
Kikundi hicho cha ushirika kina jumla ya wanachama 57 na
kinaongozwa na Bw. Malamla kama mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti ni Zuberi Luwono,
Hassan Ally Sozigwa (Katibu), na wajumbe ni Shaaban Hassan Bogoma, Ally Omari
Vullu, Suleiman Kitalambo na Juma Said Mwinyi.
Malamla anasema kwamba, kwa utaratibu waliojiwekea, kila
mwanachama kati ya hao 57 lazima kila siku achangie Shs. 4,000 ambapo Shs.
2,000 ni kwa ajili ya gesi na Shs. 2,000 kama ada.
“Utaratibu huu ni kila siku, hivyo kwa kukusanya Shs. 2,000
za ada kila siku tuna uwezo wa kuingiza Shs. 114,000 kila siku na kwa maana
hiyo kwa mwezi tunaweza kuingiza wastani wa Shs. 3 milioni.
“Tunao wasaidizi 30 wanaofanya shughuli za kuchinja pia humu
ndani, lakini hawa hawahesabiwi kama ilivyo kwa wanachama wenyewe, na mara
nyingi wasaidizi hawa huwa ni wale wanaowasaidia wanachama husika,” anaongeza.
Kwa mujibu wa Malamla, hivi sasa wanayo akiba ya kuridhisha
ingawa inaweza isitoshe kuanzisha shughuli za ufugaji mkubwa ambazo zinahitaji
fedha nyingi zaidi.
“Hatujapiga hesabu, lakini najua shughuli hizi zinahitaji
fedha nyingi zaidi, tunaamini kwa dhamira ya dhati tuliyonayo, ipo siku
tutafanikiwa tu katika mipango yetu,” anasema.
Mbali ya akiba ya fedha benki, lakini ushirika huo unamiliki
viwanja takriban 21 vyenye ‘Offer’ katika eneo la ekari 10 huko Mbutu, Kigamboni
jijini Dar es Salaam ambapo miongoni mwa viwanja hivyo ni eneo la ekari moja
ambalo wanataka waanzie ufugaji wa kuku na samaki.
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa Shirikisho la
Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Bw. Henry Mwatwinza Mwimbe, anasema kwamba,
KIPOCOSO ni miongoni mwa vyama vya ushirika vya msingi vilivyoonyesha mafanikio
makubwa katika kipindi kifupi.
“Kimeanzishwa muda mrefu, lakini kimepitia katika uongozi
mbovu ambao pengine haukuwa na malengo, uongozi wa sasa tangu ulipoingia
madarakani mwezi Machi 19, 2017 umeweza kufanya mambo makubwa sana kwa
usimamizi wetu na bado tunaendelea kuwasaidia maoni na mambo mbalimbali
kuhakikisha kwamba wanapiga hatua,” anasema Mwimbe.
Mwimbe anasema kwamba, kwa hatua waliyofikia, KIPOCOSO
wanaweza kabisa kukopesheka kwani licha ya akiba waliyonayo, bado wanayo
rasilimali ardhi na wana malengo ya kuwekeza katika kilimo na ufugaji.
Changamoto
Pamoja na mafanikio waliyonayo, lakini wajasiriamali hao wanasema kwamba, wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, hususan masuala ya usafi wa mazingira.
Pamoja na mafanikio waliyonayo, lakini wajasiriamali hao wanasema kwamba, wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, hususan masuala ya usafi wa mazingira.
Mzee Shaaban Bogoma anasema kwamba, mifumo ya majitaka
iliyowekwa na Halmashauri ya Jiji (mifumo ya DSSD) haikidhi mahitaji na wakati
mwingine mitaro hufurika na kuchafua mazingira.
“Majengo ya jirani hapa yameweka mifumo ya nje ya kumwaga
maji, sasa mvua ikinyesha maji yote yanaingia kwenye mfumo wetu na kwa vile
wakati mwingine unakuwa umeziba, basi maji hufurika na kuleta kero kubwa ndani
ya soko,” anasema Mzee Bogoma.
Kwa upande wake, Malamla anasema kwamba, bila DSSD
kurekebisha mifumo ya majitaka, hali itaendelea kuwa tete na kuhatarisha afya
za wafanyabiashara na walaji.
“Majengo mengine mara nyingi hutiririsha maji machafu kwa
muda mrefu bila watendaji wa halmashauri kufuatilia, lakini ikitokea kwamba
mfumo wetu, ambao ni mdogo na unazidiwa, ukatiririsha maji yenye damu kutokana na mitaro kuziba, hapa huwa ni mshike
mshike,” anasema.
Amezitaka mamlaka husika kuhakikisha zinawajibika kwa nafasi
zao ili kuweka mazingira bora katika soko hilo kwa kulinda afya za walaji na
wafanyabiashara kwa ujumla, kwani huduma yao ni muhimu kwa afya ya binadamu na
usafi ndiyo kipaumbele cha kwanza.
Kuhusu masuala ya utawala, Malamla ameupongeza uongozi wa
TFC kwa kutambua shida zao pamoja na kuwapa miongozo ya mara kwa mara ambayo
imezidi kuwaimarisha na kupata fikra mpya za uwekezaji.
Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Simu: +255 656 331974.
0 comments:
Post a Comment