Imeandikwa na Mwandishi Wetu
TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya
Okoa Moyo wa Mtoto (SACH) ya nchini Israel, wamefanya upasuaji wa bila
kufungua kifua (catheterization) kwa watoto 20 wenye matatizo ya moyo.
Upasuaji huo unatumia mtambo wa Cathlab, umefanyika katika kambi
maalumu ya matibabu iliyoanza Novemba 23, mwaka huu na kumalizika leo.
Matibabu yaliyofanyika ni ya kuziba matundu kwenye moyo na kutanua
mishipa ya moyo.
“Katika kambi hii tunatarajia kufanya uchunguzi wa moyo kwa watoto
100 kati ya hao watoto 60 ambao watakuwa na matatizo makubwa watapelekwa
Israel kufanyiwa upasuaji wa kufungua kifua mwakani na 40 watatibiwa
nchini,” ilieleza taarifa iliyotolewa na JKCI.
“Tumepanga kufanya matibabu kwa watoto 25. Tunaamini hadi kambi
itakapomalizika watoto wote hawa watakuwa wamepata matibabu. Watoto 20
waliopata matibabu wengine wameruhusiwa na waliobaki hali zao
zinaendelea vizuri na wataruhusiwa pindi afya zao zitakapoimarika,”
iliongeza taarifa.
Tangu mwaka 2015, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ilianza
kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (SACH) ya Israel, na hadi
sasa watoto 40 wamefanyiwa upasuaji wa moyo Israel. Gharama za matibabu
ya watoto hawa zinagharamiwa na taasisi hiyo ya JKCI. “Tunawashukuru
wenzetu hawa wa SACH kwa kuona umuhimu wa kutoa huduma ya matibabu bure
kwa watoto wenye matatizo ya moyo.
Watoto waliotibiwa wamepona na wale ambao walikuwa wanafunzi
wanaendelea na masomo yao,” iliongeza. Ilisema wakati kambi hiyo
ikiendelea, baadhi ya wafanyakazi wa SACH na JKCI walienda Kagera
kufuatilia maendeleo ya mtoto Julius Kaijage (12), mwanafunzi wa darasa
la nne Shule ya Msingi Green Acres, Bunazi aliyefanyiwa upasuaji wa moyo
Israel mwaka 2013.
“Tumekuwa na tabia ya kufuatilia maendeleo ya watoto tunaowafanyia
upasuaji hii inatusaidia kufahamu maendeleo yao,” ilieleza taarifa ya
JKCI. Taarifa ya JKCI iliongeza kuwa wanatarajia kuwa na kambi nyingine
ya matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima itakayoanza leo hadi
Desemba mosi, mwaka huu.
“Katika kambi hii ambayo tutashirikiana na wenzetu kutoka Taasisi ya
Open Heart International ya nchini Australia tunatarajia kufanya
upasuaji wa kufungua kifua kwa watoto 13 na watu wazima 10,” iliongeza
taarifa ya JKCI.
Imewaomba wananchi waendeleee kuchangia damu kwani wagonjwa
wanaofanyiwa upasuaji wa moyo wanahitaji kuongezewa damu wakati
wanapatiwa matibabu. Pia imeeleza kutokana na matibabu ya moyo kuwa ni
ya gharama, wamewahimiza wananchi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya (NHIF) ambao utawasaidia kulipa gharama za matibabu pindi
watakapougua na kuhitaji kupata matibabu.
Mbali ya hayo, Bodi ya Udhamini, uongozi na wafanyakazi wa JKCI
wamemshukuru Rais John Magufuli katika hotuba yake aliyoitoa juzi wakati
wa ufunguzi wa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na
Sayansi Shirikishi Muhimbili Kampasi ya Mloganzila kwa kuwapatia jengo
ambalo watalifanya kuwa jengo la watoto. “Kama mnavyofahamu asilimia 70
ya wagonjwa tunaowafanyia upasuaji wa kufungua kifua ni watoto, tuna
vitanda 123 kati ya hivi vitanda vya watoto ni 24 tu,” ilieleza taarifa
ya JKCI.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment