Rais
John Magufuli akitoa maelekezo kuhusu magari zaidi ya 50 yanayodaiwa
kuwa ya Polisi yaliyopo bandari ya Dar es Salaam tangu mwaka 2015 kwa
sababu ya kutolipiwa ushuru alipofanya ziara ya kushtukiza jana.
RAIS John Mafufuli ametoa siku saba kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Jeshi la Polisi kumpa
taarifa juu ya sababu za magari madogo ya kubebea wagonjwa 50 na magari
ya Jeshi la Polisi 53 kukwama Bandari ya Dar es Salaam kwa miaka miwili
sasa huku baadhi yakiwa yamedaiwa kuingizwa kwa jina la Ofisi ya Rais
wakati yeye hajui.
Jana, Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika maeneo ya
kutunzia magari ndani Bandari ya Dar es Salaam na kubaini uwepo wa
magari madogo ya kubebea wagonjwa 50 ambayo yamekwama bandarini hapo
tangu Juni, 29, 2015 na magari ya Jeshi la Polisi 53 ambayo yamekwama
tangu Juni 2016. Dk Magufuli pia amebaini uwepo wa magari
yaliyotekelezwa bandari hapo kwa zaidi ya miaka 10 hali inayopunguza
uwezo wa bandari kuhifadhi mizigo.
Kutokana na hali hiyo, ametoa siku saba kwa TRA, TPA na Jeshi la
Polisi kumpa taarifa juu ya sababu za magari hayo kukwama bandarini hapo
kwa muda mrefu na kinyume cha sheria na kumtaja mmiliki wake na pia
ameagiza magari yote ambayo yamekaa bandarini hapo kwa muda mrefu
yaondolewe kwa taratibu za kisheria na kwa uwazi kutoa nafasi zaidi.
“Nataka magari yote yaliyokaa muda mrefu kupita muda uliopangwa
kisheria yaondolewe haraka, kama ni kupigwa mnada yapigwe mnada, kama ni
kuchukuliwa na Serikali yachukuliwe, hatuwezi kuendelea kutunza magari
ya watu humu kwa miaka 10 tena watu wengine hawajulikani,” aliagiza Rais
Magufuli.
Rais Magufuli pia amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kamishna wa Polisi, Valentino Mlowola
kuchunguza magari yote yaliyokwama bandarini baada ya kuagizwa kwa
majina ya taasisi za Serikali (Rais) na kuwabaini walioshiriki katika
uingizaji.
Rais Dk Magufuli aliyeongozana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk
Philip Mpango aliwataka mawaziri hao kufuatilia utendaji kazi wa vyombo
na taasisi wanazozisimamia na kuchukua hatua wanapobaini mambo
yasiyofaa.
Pia Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta
Jenerali Simon Sirro kuyakagua magari 53 ya Polisi ambayo yamekaa muda
mrefu bandarini bila kutolewa. Alimtaka IGP Sirro kuondoa mianya ya
rushwa Polisi huku akimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishna wa
Polisi, Mlowola kuchunguza mazingira ya uagizwaji magari hayo ya Polisi
na kukwama.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment