Mkurugenzi
wa Idara ya habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan
Abbas akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari kwenye ukumbi wa Idara
ya Habari Maelezo wakati alipotoa taarifa ya utekelezaji wa miradi
mbalimbali inayotekelezwa na serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Rais Dkt. John Pombe Magufuli na kutolea
ufafanuzi wa masuala kadhaa, Pichani kushoto Mkurugenzi Msaidizi
upande wa usajiri wa Magazeti Ndugu Patric Kipangula na
Kulia Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Maelezo, Rodney Thadeus
Mkurugenzi
wa Idara ya habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan
Abbas akifafanua jambo kwa Waandishi wa habari mapema leo katika ukumbi
wa Idara ya Habari MAELEZO,alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa
miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ya awamu ya Tano chini ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania,Dkt. John Pombe Magufuli.
Pichani kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi upande wa usajiri wa Magazeti
Ndugu Patric Kipangula na Kulia Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Maelezo, Rodney Thadeus .PICHA NA MICHUZI JR
NIDHAMU
mpya katika ukusanyaji na matumizi ya fedha za umma na dhamira ya dhati
ya kutekeleza ahadi kubwa kwa faida ya wananchi vimesaidia Serikali ya
Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuendelea kutekeleza kwa mafanikio miradi
mbalimbali mikubwa ya kitaifa. Baadhi ya mambo yaliyotekelezwa na
kufafanuliwa leo kwa wanahabari ni kama ifuatavyo:
Hali ya Uchumi
Kama
alivyoeleza Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango siku
chache zilizopita, tunawahakikishia watanzania kuwa hali ya uchumi wa
nchi yetu inaendelea kuwa imara kwa kiasi cha kuziridhisha taasisi
mbalimbali za kimataifa.
Ripoti
za Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya Dunia (WB) na Taasisi ya
Goldman Sachs ya Marekani zimetabiri kuwa wakati uchumi wa dunia utakua
kwa wastani wa asilimia 3.0 hadi 4.0, ukuaji wa uchumi wa Tanzania
unatajwa kuendelea kuwa kati ya nchi tano bora za Afrika ukitarajiwa
kukua kwa asilimia 6.5 hadi 7.0 katika mwaka 2018.
Ahadi ya Kuhamia Dodoma
Serikali
ya Awamu ya Tano imeendelea kuonesha nidhamu ya kuahidi na kutekeleza
ahadi ya kuhamia makao makuu, Dodoma. Kufikia mwishoni mwa Desemba,
2017, viongozi waandamizi wa Serikali wameshahamia Dodoma. Rais mwenyewe
akitarajiwa mwaka huu.
Mbali
na viongozi, jumla ya wafanyakazi 3,671 kutoka wizara na taasisi
mbalimbali za umma wameshahamia makao makuu Dodoma. Awamu inayofuata
baadaye mwaka huu itahusisha wafanyakazi wengine 2,460. Sekta binafsi
ichangamkie fursa za Dodoma.
Viwanda Vyashamirisha Uchumi Mpya
Moja
ya ajenda kuu za Serikali ya Awamu ya Tano ni kujenga uchumi mpya wa
viwanda. Kufikia mwaka jana viwanda zaidi ya 3,300 vilisajiliwa kupitia
Msajili wa Makampuni (250), Kituo cha Uwekezaji (361), Mamlaka ya
Usimamizi wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi (41) na Shirika la Kuhudumia
Viwanda Vidogo (SIDO lililosajili viwanda vidogo vya kati ya mtu mmoja
hadi 9 takribani 2,721). Ujenzi na uzalishaji katika viwanda hivi uko
katika hatua mbalimbali.
Kati
ya miradi hiyo iliyosajiliwa, viwanda vikubwa ni 652. Viwanda hivi vina
jumla ya mtaji wa zaidi ya TZS trilioni 5 utakaowekezwa nchini na
vitaajiri watu 50,625. Katika taarifa ya mwezi ujao tutaainisha baadhi
ya viwanda vilivyokamilika na uzalishaji unavyoendelea.
Miradi Mikubwa ya Umeme
Katika
sekta ya nishati, Serikali inaendelea kutekeleza miradi zaidi ya 20 ya
kuhakikisha nchi ina umeme wa uhakika. Miongoni mwa miradi ya kimageuzi
ni usimikaji wa mitambo ya umeme wa gesi Kinyerezi I (mtambo wa nyongeza
wa megawati 185) na Kinyerezi II wa megawati 240. Mitambo hii kwa
pamoja itaongeza megawati 425.
Mtambo
wa Kinyerezi 1-nyongeza umefikia asilimia 50. Mtambo wa Kinyerezi II
umekamilika kwa asilimia 87 ambapo Desemba, 2017, mtambo huo wa kisasa
umeingiza megawati 55.94 katika gridi ya Taifa. Kiasi kingine cha
megawati 27.94 kinatarajiwa kuingia kwenye gridi mwezi huu. Mitambo yote
miwili itakamilika mwaka huu.
Ujenzi Reli ya Kisasa “Standard Gauge”
Aidha,
Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya
kisasa kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge) kwa kuanzia na
kipande cha kilometa 300 (Dar-Moro) kitakachogharimu TZS trilioni 2.7.
Kazi
ya kusanifu njia yote itakayopita reli imeshakamilika na kwa sasa
uandaaji wa tuta, ujenzi wa madaraja kabla ya kutandika reli yenyewe
umeanza kwa kasi. Aidha, ujenzi wa kipande cha pili cha kilometa 442
(Morogoro-Makutupora, Dodoma) kitakachogharimu TZS TZS trilioni 4.3,
mkandarasi ameshaanza maandalizi.
Ununuzi Mabehewa, Vichwa Waanza
Wakati
ujenzi wa reli ukiendelea, Serikali kupitia Kampuni Hodhi ya Raslimali
za Reli (RAHCO) imeshatangaza zabuni kwa ajili ya kupata makampuni
yatakayotengeneza vichwa na mabehewa ya kisasa ya treni ya umeme na
mafuta. Zabuni zitafunguliwa mwezi huu.
Katika
zabuni hiyo Serikali inatarajia kununua vichwa 25 (23 vya umeme na 2
vya dizeli), mitambo 25 ya ukarabati wa reli na mabehewa 1,590 (kati ya
hayo 1,530 yakiwa ni ya aina mbalimbali za mizigo kama vile kubeba
makontena, nafaka, mafuta n.k), mabehewa 60 ni ya abiria (15 yakiwa ni
daraja la kwanza na 45 daraja la kawaida).
Meli Mpya Zaleta Matumaini Maziwa Makuu
Serikali
iliahidi na sasa inatekeleza. Katika Ziwa Nyasa mwishoni mwa wiki
iliyopita meli mbili mpya za mizigo za MV Njombe na MV Ruvuma zinazobeba
mizigo tani 1,000 kila moja zimeanza safari kwenda bandari mbalimbali
zikiwemo za nchi jirani. Serikali imetumia TZS Bilioni 11.252 na meli
nyingine mpya ya abiria itakamilika Juni mwaka huu.
Katika
Ziwa Victoria, kupitia kampuni ya Serikali ya Huduma za Usafiri Katika
Maziwa, Marine Services Company LTD, mkandarasi wa kutengeneza meli
mbili kubwa, mpya na za kisasa ameshapatikana. Aidha, tayari meli ya
abiria ya MV Clarios na ya mizigo MV Umoja zilizofanyiwa ukarabati na
kuwa za kisasa zimeshaanza kazi.
Katika
taarifa zijazo tutaendelea kutoa maendeleo ya miradi hii mikubwa na
kuainisha utekelezaji katika sekta na miradi mingine kwa wananchi. Kwa
maelezo zaidi kuhusu taarifa ya leo ikiwemo picha za miradi
zinazoambatana na taarifa hii tafadhali tembelea:
Tovuti: www.maelezo.go.tz
Blogu: www.blog.maelezo.go.tz
Twitter: TZ_Msemaji Mkuu
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.
0 comments:
Post a Comment