Kamishna
wa Kodi za Ndani, Elijah Mwandumbya (kulia)akizungumza na Waandishi
wa Habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es Salaam kuhusu uzinduzi wa
Kampeni ya Usajili wa Walipakodi.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imeondoa utaratibu wa awali kwa walipakodi
wadogo kulipia kodi kabla ya kuanza kufanya biashara na badala yake
kuwataka kulipia robo ya kwanza ndani ya siku tisini tangu kusajiliwa.
Kamishna
wa Kodi za Ndani, Elijah Mwandumbya ameyabainisha hayo leo Jijini Dar
es Salaam wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi
wa Kampeni ya Usajili wa Walipakodi.
Mwandumbya
amesema jukumu la usajili wa walipakodi kwa Mamlaka hiyo ni chanzo cha
kuongeza idadi ya walipakodi, wigo wa ulipaji kodi, kuongeza makusanyo
pamoja na kuwa na taarifa sahihi za walipakodi wanaostahili kukadiriwa
na kutozwa kodi ili kuchangia Pato la Taifa.
“kampeni
hii inaenda sambamba na mabadiliko makubwa tuliyoyafanya kwa walipakodi
wadogo kwa kuwapa siku tisini za kulipa kodi kwa robo ya kwanza ya
malipo pindi tu watakapokuwa wamesajiliwa hivyo mabadiliko hayo yatakuwa
chachu katika usajili kwani tunatarajia kusajili walipakodi takribani
milioni moja nchi nzima,”alisema Mwandumbya.
Kamishna
wa Kodi za Ndani amesisitiza kuwa usajili wa TIN ni bure na utafanyika
katika ofisi zote za Mamlaka hiyo na katika vituo maalum vitakavyokuwa
vimeteuliwa na kutangazwa kupitia vyombo vya habari na matangazo katika
maeneo husika.
Aidha,
Mwandumbya amewataka wananchi kujihadhari na vishoka wanaoweza kutumia
mwanya wa kuharibu nia njema ya kampeni hiyo kwani hakuna wakala yeyote
aliyepewa jukumu la kusajili wala kutoa fomu za usajili wa zoezi hilo.
Amefafanua
kuwa muhusika lazima aende mwenyewe ili apigwe picha na kuchukuliwa
alama za vidole pia atatakiwa aende na mkataba wa pango au uthibitisho
wa umiliki wa mahali pa biashara, barua yenye muhuri na namba ya simu ya
Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa pamoja na kitambulisho cha muhusika
kama vile hati ya kusafiria, leseni ya udereva, kitambulisho cha uraia
au cha mpiga kura.
Kampeni
hiyo imezinduliwa nchi nzima kwa nia ya kuhakikisha kila mwananchi
anayestahili kupatiwa namba ya utambulisho ya mlipakodi anasajiliwa na
kupata namba hiyo kwa urahisi na haraka.
0 comments:
Post a Comment