Chama
cha Mapinduzi (CCM), kimesema kipindi hiki cha msiba wa mwanasiasa
mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru ndicho cha kuvieleza vyama
vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Siha na
Kinondoni kufanya kampeni safi.
Wakati
chama hicho kikisema hayo kupitia kwa katibu wake wa itikadi na uenezi,
Humphrey Polepole, chama kingine kinachoshiriki kampeni hizo, Chadema
kimesema kitasimamisha shughuli zote za kampeni Jumatatu siku ambayo
mwanasiasa huyo atazikwa katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Kauli
ya vyama hivyo imetokana na wito uliotolewa na Kiongozi wa Chama cha
ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe kwa vyama hivyo kusimamisha kampeni hizo
kwa siku tatu kuomboleza kifo cha mwanasiasa huyo mkongwe nchini
kutokana na mchango wake katika siasa za nchi na zaidi ndani ya vyama
hivyo.
“Kingunge
amesaidia kuimarisha CCM na baadaye akasaidia Chadema. Sioni busara
vyama kuendelea na kampeni. Nawaomba wasitishe leo (jana), kesho (leo)
na Jumatatu mwanasiasa huyu akizikwa wataendelea,” alisema jana nyumbani
kwa marehemu, Kijitonyama, Dar es Salaam.
Alipoulizwa
kuhusu wito huo, Polepole alisema kwa kuwa mwanasiasa huyo ameishi na
kufa akiamini katika siasa za ujamaa na kujitegemea ambazo msingi wake
ni kufanya kazi, huu si wakati wa kusimamisha kampeni.
“Ni
wakati wa kueleza kuwa vyama vya siasa vina jukumu la kufanya kampeni
safi, kujenga misingi imara ya kuwapata makada na wanachama wanaosimamia
kwenye imani ya vyama vyao na kuwapata viongozi bora.”
Alisema kazi kubwa aliyoifanya Kingunge tangu kuasisiwa kwa Taifa hadi alipofariki, inapaswa kuendelezwa.
“Nanukuu
kifungu cha Biblia ‘mbio amezipiga na mwendo ameumaliza’. Hivyo
Kingunge ameumaliza mwendo kazi kubwa ni kuendeleza mema na mazuri
aliyotenda,” alisema Polepole.
Mkurugenzi
wa itifaki, mawasiliano, uenezi na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema
alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu ombi hilo la Zitto alisema chama
hicho kitasitisha kampeni zake kesho.
“Huu
ni ushauri, na mzee wetu amefariki dunia kampeni zikiwa zimeanza na
zinafanyika kwa muda mfupi kabla ya uchaguzi. Tuliona Jumatatu (kesho)
ndio tushiriki kikamilifu kumuaga mzee wetu na hatutafanya kampeni.”
Hata
hivyo, Mrema alisema awali kwamba ni vigumu kutoa uamuzi kuhusu ushauri
huo wa Zitto kwa kuwa suala hilo linapaswa kutolewa tamko baada ya
vikao kauli inayofanana na ya mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
“Leo
(jana) baada ya kampeni tutafanya kikao cha tathmini lakini ni kwamba
sisi tuliona Jumatatu kuwa siku muafaka kutofanya kampeni ili kushiriki
shughuli ya kumhifadhi mzee wetu,” alisema Mrema huku Mbowe akisema,
“Hili ni swali gumu, lakini nitakwenda kushauriana na viongozi ili tujue
cha kufanya.”
Vyama
takriban 12 vipo katika kampeni za ubunge jimbo la Kinondoni, Dar es
Salaam na Siha, Kilimanjaro zilizoanza Januari 21 zikitarajiwa
kumalizika Februari 16 huku uchaguzi katika majimbo hayo na kata 10
ukitarajiwa kufanyika Februari 17.
Kingunge
aliyekuwa kada wa CCM mwenye kadi namba nane, alitangaza kukihama chama
hicho Oktoba 4, 2015 na kusema hatajiunga na chama chochote lakini mara
kadhaa alionekana akipanda majukwaa ya upinzani kumnadi aliyekuwa
mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa kwenye Uchaguzi Mkuu
uliofanyika Oktoba 25, 2015.
Mwanasiasa
huyo alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
ikiwa ni mwezi mmoja baada ya mkewe, Peras kufariki katika hospitali
hiyohiyo.
0 comments:
Post a Comment