Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeridhia kuhamishwa kwa vituo 46 vya
kupigia Kura katika kata tatu za jimbo la Kinondoni zitakazofanya Uchaguzi mdogo
wa Ubunge Februari 17 mwaka huu.
Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Ramadhani Kailima ameeleza kuwa uamuzi wa NEC
kuridhia kuhamishwa kwa vituo hivyo, umetokana na makubaliano yaliyofikiwa
katika Mkutano wa Msimamizi wa Uchaguzi wa
jimbo la Kinondoni na Vyama vya siasa
juu ya kuhamishwa kwa vituo hivyo vilivyokuwa kwenye nyumba za Ibada, Zahanati
na maeneo ya majengo ya watu binafsi.
Amesema Tume imeridhika na uamuzi huo kwasababu hatua zilizochukuliwa ni
sahihi kwa mujibu sheria na kanuni namba 21 ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu
la Wapiga Kura ambayo inaeleza kuwa ;
Vituo vya Kupigia Kura havitakiwi kuwekwa katika majengo ya nyumba za
Ibada, kambi za jeshi, nyumba za watu binafsi na ofisi za vyama vya siasa.
“ Tumejiridhisha kuwa baadhi ya vituo katika Kata ya Kigogo vilikuwa katika nyumba za Ibada na vingine
kuwa katika maeneo yenye ufinyu wa nafasi hivyo tumeridhia vituo hivyo vihamishwe
na kupelekwa katika majengo ya umma” Amesema.
Amesema kuwa baadhi ya vituo vya kupigia Kura vilivyokuwa katika majengo
ya umma ikiwemo Zahanati vimehamishwa katika shule za msingi za umma zilizo
katika kata hizo ili kuondoa usumbufu
kwa wagonjwa.
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Mwananyamala Bi. Barima Omari
ameeleza kuwa kata ya Mwananyamala ina vituo vya kupigia kura 65 na wapiga kura
27,589 na kuongeza kuwa vituo nane (8) vilivyokuwa katika shule ya Sekondari
Kambangwa mtaa wa msisiri A vimehamishwa. Kati ya hivyo 6 vimehamishiwa katika Ofisi
ya Serikali ya Mtaa ya Msolomi na 2 kuhamishiwa uwanja wa kwakopa.
Naye Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi
Kata ya Kijitonyama Elizabeth Minga ameeleza kuwa Kata hiyo ina jumla ya
vituo vya kupigia Kura 101, kati ya hivyo vituo 22 vimehamishwa.
Akifafanua kuhusu vituo hivyo amesema vituo 6 vilivyokuwa katika shule
ya Sekondari Kenton vimehamia shule ya Msingi Mapambano na vituo 5 vilivyokuwa
nje ya Ofisi ya serikali ya Mtaa wa Bwawani vimehamishiwa mbele ya ofisi hiyo.
Aidha,
vituo 6 vilivyokuwa nje ya
soko la Makumbusho vimehamia ndani ya Ofisi ya Meneja wa Soko hilo na
vituo 5 vilivyokuwa katika Ofisi ya Serikali za mitaa kijitonyama
vimehamishiwa katika shule ya msingi kijitonyama.
Kwa upande wake Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Kigogo Bw. Singoro
Mdegela ameeleza kuwa kata yake ina idadi ya Wapiga kura 27,000 na Vituo vya
Kupigia Kura 59.
Amesema katika Kata hiyo vituo 16 vimehamishwa ambapo vituo 5
vilivyokuwa eneo la Kiwenge kwenye Msikiti wa Shiha vimehamia Uwanja wa People
na Vituo 6 vilivyokuwa kwenye Zahanati ya Kigogo vimehamishiwa katika Shule ya
Msingi Kigogo ili kuruhusu shughuli za matibabu kwa wagonjwa kuendelea.
Aidha, vituo 5 katika ofisi ya serikali ya mtaa wa Mkwajuni vimehamishiwa
katika shule ya secondari Kigogo.
0 comments:
Post a Comment