Na. OWM - KAM (DSM)
Mamia
ya Vijana kutoka Mikoa mbalimbali nchini wamejitokeza katika Chuo cha
Taifa cha Usafirishaji (NIT) kushiriki zoezi la usajili wa madereva
wanaotarajia kwenda kufanya kazi nchini Qatar.
Zoezi
hili ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya Serikali ya kuwaunganisha
Watanzania na fursa za Ajira nje ya nchi kupitia mifumo rasmi ili
kuhakikisha ulinzi wa haki na usalama wao.
Kaimu
Mkurugenzi wa Huduma za Ajira, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na
Mahusiano Jane Sorogo, amebainisha kuwa mwitikio umekuwa mkubwa ambapo
zaidi ya Vijana 1,700 wamejitokeza kuomba nafasi hizo licha ya mahitaji
kuwa ni madereva 1,500 pekee.
Akizungumza
wakati wa ziara yake chuoni hapo tarehe 06 Februari 2026, Waziri wa
Nchi hiyo Mhe. Clement Sangu, amesema Serikali imeweka mifumo imara ya
kisheria inayosimamia Ajira hizo ili kulinda maslahi ya Watanzania.
Waziri
Sangu pia amebainisha kuwa tangu mwezi Novemba 2025 hadi Januari 2026,
jumla ya Watanzania 2,019 wameunganishwa na fursa za Ajira katika nchi
za Saudi Arabia, Qatar, Oman, Falme za Kiarabu na kwingineko.
Aidha, amesema Serikali iko mbioni kusaini hati za makubaliano na nchi nyingine 16 ili kuzidi kutanua wigo wa Ajira kwa vijana.
Mhe.
Sangu ametoa wito kwa vijana kuendelea kuchangamkia fursa hizo kupitia
njia rasmi za Serikali na kuepuka mawakala wasio rasmi kwa maslahi ya
usalama wao na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza
kwa niaba ya waombaji, mmoja wa madereva waliojitokeza, Hassan Mohamed,
amesema ameamua kufuata utaratibu huo rasmi kwa kuwa unatoa uhakika wa
ulinzi wa haki na maslahi yake akiwa ugenini.
Juhudi
hizi zinaonyesha dhamira ya Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu
katika kutengeneza mifumo inayotoa matumaini na usalama kwa nguvu kazi
ya kitanzania inayotafuta fursa nje ya mipaka.



0 comments:
Post a Comment