Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » DAR YAVUNJA REKODI MIMBA ZA UTOTONI (2)

DAR YAVUNJA REKODI MIMBA ZA UTOTONI (2)

 
Baadhi ya wanafunzi wa kike wakiwa katika moja ya mikutano kuhusiana na udhalilishaji wa kijinsia. Picha ya Maktaba. 
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni ya kuzuia matukio ya ujauzito kwa watoto wa kike hali si ya kuridhisha.
Mwaka 2011 idadi ya wanafunzi waliopata ujauzito ilikuwa ni 13,146, 2012 ikashuka hadi kufikia 11,419, lakini kwa mwaka 2013 idadi hiyo iliongezeka na kufikia 21,420.
Pamoja na kuwepo kwa sababu mbalimbali zinazotajwa kuwa chanzo cha mimba hizo hususani kwa maeneo ya mijini ni madereva bodaboda na pamoja na makondakta wa daladala.
Uchache wa maeneo ya ndani ya miji umekuwa ni chanzo cha uanzishwaji wa shule za pembezoni.
Sasa kutokana na mbali wa maeneo zilizopo shule hizo, watoto hulazimika kutumia vyombo vya usafiri wakati wa kwenda na kurudi shuleni.
Kwani si jambo rahisi kwa watoto hawa kufika maeneo kama Msongola, Chanika, Mvuti na mengineyo.
Sasa kwa kuwa usafiri unakuwa sehemu ya maisha yao, madereva na makondakta hao hutumia njia mbalimbali kuwarubuni, matokeo yake ni kupatikana kwa hizo mimba tunazozungumzia.
Je, makondakta na madereva hao wanaliongeleaje suala hilo?
Juma Mkumba (42) ni dereva wa daladala zinazofanya safari zake ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Anasema hapingani na kauli iliyotolewa na mkuu wa mkoa kuwa madereva na makondakta ni miongoni mwa vyanzo vya mimba hizo.
Pamoja na kuwa kitendo hiki hakipendezi hata kidogo kukisikia masikioni, lakini ukweli ni kwamba haya matukio yapo.
“Tumeshuhudia vijana wengi wakianzisha uhusiano na watoto wa kike. Na pia tumejionea wenyewe wasichana hawa wanavyoishia kukatiza ndoto za maisha yao kwa kupata ujauzito. Kama mzazi sifurahishwi kabisa na jambo hili, kwani licha ya kuleta picha mbaya kwa jamii pia hukwamisha ustawi wa mtoto wa kike na taifa kwa ujumla” anasisitiza Mkumba.
Wito wangu kwa serikali ni kuwachukulia hatua wale wote wanaowarubuni watoto hawa na hata kuwaharibia maisha yao anasisitiz 
Gazeti hili pia lilifanikiwa kuongea na madereva wa bodaboda kutaka kujua mtazamo wao juu ya kauli ya mkuu wa mkoa. Kassim Hairun (25) wa Mbagala Kingugi akiwa miongoni mwa madereva wa pikipiki wa muda mrefu anasema kwamba, kiongozi huyo yupo sahihi kabisa.
Hata hapa ninapoongea na wewe, wapo madereva wenzetu wanaojihusisha na uhusiano na watoto hao, cha kusikitisha zaidi ni kuwa licha ya kuwaweka kwenye hatari ya kupata ujauzito, pia watoto hawa wako hatarini kupata magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya zinaa ukiwamo Ukimwi.
“Kutokana na udogo watoto hawa hushindwa kutoa uamuzi kuhusiana na matumizi ya njia za uzazi wa mpango, kwa maneno rahisi tunaweza kusema, hapa mtoto huyu asiye na hatia hujikuta akiingia kwenye janga linalosababishwa na tamaa za watu hawa wasio na hata chembe ya huruma,” anafafanua.
Kinachokera zaidi ni kule kujiweka pembeni kwa jamii. Maana wawili hawa wanapokubaliana, si kweli kuwa huwa wanaenda kutimiza uhalifu huo maporini. Huwenda kwenye nyumba za wageni au wakati mwingine kwenye makazi yao, ambako kote kumezungukwa na jamii.
“Hivi ingekuwa sheria zinafuatwa ipasavyo, ni wapi ingepatikana sehemu ya kufanyia uhalifu huu,” anahoji.
Pamoja na mitazamo ya watu mbalimbali kuhusiana na tatizo hilo waathirika wa tatizo hili wengi wao wameonekana kujutia, wakiongea na gazeti hili kila mmoja kwa wakati wake anasema kuwa angejua ni nini kingetokea asingethubutu kuingia kwenye janga hilo. Zainab Matilga (18) ni mmoja wa wanafunzi hao. Yeye alichaguliwa kwenye shule ya Jangwani mara baada ya kufaulu Shule ya Msingi Kilakala iliyopo Yombo wilayani Temeke.
“Nilipachikwa ujauzito nikiwa kidato cha pili, wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 16 tu, ndoto yangu ya kuwa daktari ilizimikia hapo kwani sikuweza kuendelea tena na shule,” anafafanua.
“Kijana mmoja mwendesha bodaboda ndiyo alikuwa baba wa mtoto,” anasema.
Anasema hawezi kusahau katika maisha yake, kwani baada ya kupata ujauzito huu, wazazi wake walimfukuza nyumbani, hivyo akaamua kwenda kuishi na kijana aliyempa mimba hiyo.
“Maisha yalikuwa magumu sana, mtoto wangu alidhoofika na baadaye alifariki dunia kwa malaria.” Anaongeza, “Baada ya kifo chake niliamua nirudi nyumbani na kuomba radhi wanipokee niendelee na masomo lakini hakuna aliyenisikiliza, matokeo yake nilirudi mtaani na kujikuta nikipachikwa mimba nyingine. Hivi sasa nina miaka 18 na tayari nina mtoto mwingine wa pili,” anasisitiza Zainab.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sophia Mjema, anasema kuwa, mimba katika umri mdogo ni tatizo linalozikabili wilaya mbalimbali nchini ikiwamo Temeke.
“Tumekuwa tukifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha tatizo hili linakuwa historia, lakini ili tufanikiwe, juhudi za mtu mmoja mmoja zinahitajika” anafafanua.
Yeyote atakayejihusisha na uhusiano na watoto hawa achukuliwe hatua za kisheria. Lakini pamoja na hilo, jamii ijikite katika kutoa sapoti katika mapambano dhidi ya mimba kwa watoto nchini.
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa