Home » » HALMASHAURI YA JIJI LA DAR ES SALAAM YAPANDISHA GHARAMA ZA UZOAJI TAKA

HALMASHAURI YA JIJI LA DAR ES SALAAM YAPANDISHA GHARAMA ZA UZOAJI TAKA




NA MWANDISHI WETU


BAADA ya Halmashauri ya Wilaya ya Ilala
jijini Dar es Salaam kupandisha gharama za kuzoa taka katika Kata kumi za
wilaya hiyo, wananchi wamedai ni baada ya kiongozi mmoja kuchukua tenda ya
kufanyakazi hiyo.
Akiongea na mtandao wa Fullshangweblog hivi karibuni jijini Dar es salaam  amesema kuwa  madai hayo
yanatokana na kauli ya kiongozi huyo kuonekana akilazimisha malipo hayo hadi
kufikia hatua ya kutoa vitisho kwa wakazi wa kata hizo kuwa endapo yupo
anayepinga gharama hizo ni vema akaamua kuhamia katika wilaya nyingine anakoona
kuna gharama nafuu.

Gharama za kuzoa taka katika kata hizo zimepanda
kwa zaidi ya asilimia 200 ambapo imekuwa mzigo mkubwa kwa wananchi ambao maisha
yao ni ya kubahatisha katika kujiingizia kipato.

Kata ambazo zinapinga gharama hizo ni pamoja
na Kivukoni, Kisutu, Mchafukoge, Upanga Mashariki na Upanga Magharibi zote hizo
zimetakiwa wakazi wake kulipa shil. 15,000 kwa mwezi baadala ya shil. 5000

Nyingine ni Kata za Grezani, Kariakoo,
Mchikichini, Ilala na Jangwani ambapo katika gharama hizo mpya zinapaswa kulipa
shil. 10,000, ongezeko ambalo wanalipinga.

Mmoja wa madiwani wa Kata hizo ambaye hakupenda
kutajwa jina gazetini alikana kujua chochote kuhusu kiongozi huyo bali
anachojua ni wananchi kupinga kiwango cha gharama hizo kwa madai kuwa hakiendani
na hali halisi ya maisha yao.

Diwani huyo alisema haridhishwi na utaratibu
wa uongozi wa ngazi za juu kwa kupitisha kanuni na sheria zinazowahusu wakazi
wa wilaya hizo bila ya wao kushirikishwa.

“Unajua sisi madiwani tumekuwa tukifanywa
kama ‘Rabber Stampa’ wakusimamia yale yaliyokwishapitishwa na wakubwa japo
hayana maslahi kwa wananchi waliotuchgua”alilalamika diwani huyo.

Naye Mohamedi Hamisi mkazi wa moja ya kata hizo
alisema wanaamini kuwa yupo kiongozi bila kumtaja jina kwamba ndio chanzo cha
wao kuongezewa gharama haswa baada ya kupenyeza kampuni yake katika zabuni ya
kusimamia usafi katika kata hizo.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu madai hayo
ya wakazi wa kata hizo, Mkurugezi wa Wilaya hiyo, Gabriel Fuime alisema haamini
kama habari hizo zina ukweli ndani yake.


Alisema lengo la kupandisha gharama hizo
limetokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji mara kwa mara ambapo pia
zitasaidia kuboresha hali ya utendaji kazi katika kuziweka kwenye usafi zaidi
kata hizo.

Habari kwa Hisani ya Full Shangwe blog

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa