na Elizabeth John
BONDIA
mahiri wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka ‘SMG’, jana amesaini mkataba
wa pambano la kuwania ubingwa wa mabara unaotambuliwa na IBF, dhidi ya Bernard
Simon, ambalo linatarajiwa kufanyika jijini Berlin, Ujerumani Novemba 17 mwaka
huu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, wakati wa kusaini mkataba
huo, Meneja wa Cheka, Juma Mabakila, alisema pambano hilo ni la kufuzu kuingia
kwenye ‘chati’ ya mabondia 15 ambao wataiwakilisha dunia.
Cheka
ameingia mkataba na kampuni za Jambo Concepts, International Boxing Federation
(IBF), Tanzanite Sports Promotions Management, Kitwe General Traders na Louaa
Boxing Promotions ya Misri, ambayo watashirikiana kwa mwaka mmoja kumtafutia
pambano kila baada ya mwezi mmoja.
Naye
Rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TBPO), Onesmo Ngowi,
alisema baada ya pambano hilo, Cheka atapanda tena ulingoni Novemba 27
kupambana na bondia Amin Said wa Uarabuni katika pambano lisilo na ubingwa.
“Cheka
ni bondia ambaye Watanzania wengi tunamtegemea na tunajua kabisa kama ni bingwa
wa Afrika, hivyo naamini hawezi kutuangusha katika hilo, Watanzania tunatakiwa
kumuombea,” alisema Ngowi.
Kwa
upande wake, Cheka alisema, yeye siku zote huwa si muongeaji, bali mikono ndiyo
inazungumza na anaamini ataiwakilisha vizuri Tanzania na Watanzania wategemee
vitu vizuri kutoka kwake.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment