na Lucy Ngowi
BARAZA
la Habari nchini (MCT), limezindua mashindano ya waandishi wa habari kwa mwaka
2012.Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa waandishi wote wanaalikwa kupeleka kazi zao zilizochapishwa, ama kurushwa kwa njia ya redio au televisheni kuanzia Januari mosi mwaka huu hadi Desemba mwaka huu.
“Tumewaita kuwaambia dimba limeanza kwa ajili ya kupata waandishi bora wa mwaka 2012. Mwisho wa kupokea kazi hizo itakuwa ni mwishoni mwa Januari mwakani,” alisema.
Alisema kwa yeyote atakayependa kushiriki fomu zinapatikana katika tovuti ya MCT na mashirika yote yanayofadhili mashindano hayo.
Alibainisha kuwa, sherehe za kuwapata washindi zitafanyika Machi 29, mwakani.
Kwa upande wake, Meneja Uthibiti na Viwango wa MCT, Pili Mtambalike, alitaja vipengele vitakavyokuwepo katika mashindano hayo kuwa ni utawala bora, jinsia, uchumi, biashara na kilimo, michezo na utamaduni, ukimwi na maambukizi ya virusi vya ukimwi, habari za watoto na elimu.
Vingine ni mpigapicha bora, wachora vibonzo, sayansi na teknolojia, watu wenye ulemavu, majanga, matatizo, malaria, utalii na masuala ya uhifadhi, mwandishi aliyetukuka katika uandishi pamoja na makala ambazo hazitakuwa kwenye vipengele vilivyotajwa.
Alisema zawadi mbalimbali zitatolewa kwa waandishi hao ikiwa ni pamoja na cheti, vifaa vya kazi, laptops, televisheni, radio pamoja na vinasia sauti.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment