Oliver Oswald na Ivilla Mgala,
Dar es Salaam
CHAMA cha Wafanyabiashara wa simu nchini
kimeandaa mkakati maalum kwa ajili ya kutokomeza simu bandia zinazouzwa na
baadhi ya wafanyabiashara wajanja nchini.
Akizungumza Dar es Salaam jana na MTANZANIA, Katibu wa wafanyabiashara hao,
Sued Chemchem, alisema kutokana na kuenea kwa simu bandia, kumesababisha soko
la bidhaa hizo kukosa wateja wa uhakika.
Alisema wafanyabiashara wajanja kwa kiasi kikubwa wamechangia kudidimiza soko
la ndani kutokana na wateja wengi kukosa imani na simu hizo.
“Sisi kama wafanyabiashara tunawaomba hao wanaofanya mchezo huo kuacha kwani
wanaturudisha nyuma kimaendeleo na kutukosesha wateja,” alisema Chemchem.
Alisema kutokana na kukithiri kwa uuzaji wa simu bandia, wameiomba mamlaka
inayohusika kuhakikisha inatokomeza simu hizo madukani, ikiwa ni pamoja na
kuwachukulia hatua kali wanaojihusisha na vitendo hivi.
“Hali hii imekuwa ikituumiza sisi kama wafanyabiashara, kwani wengine wanabuni
mbinu za kutengeneza simu za bandia, hivyo sisi tukiagiza mzigo na kuleta
nchini unatoka kwa kusuasua kwa kuwa wajanja wanaouza simu za bandia wanauza
kwa bei ndogo,” alisema Chemchem.
Chemchem alisema chama chao kimelenga kuwakomboa wafanyabiashara wadogo wasio
na mitaji kwa kuwawezesha kufikia malengo ya kibiashara, ikiwa ni pamoja na kuwapa
mbinu bora za kujikomboa kiuchumi.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment