KIJANA aitwaye Priscus Mushi, mkazi wa Mbezi jijini Dar ambaye ni
muumini wa Kanisa la Efatha linaloongozwa na Mchungaji Josephat Mwingira
ameanika masikitiko yake baada ya kutengwa na baadhi ya ndugu kufuatia
kuoa mlemavu wa ngozi ‘albino’ aitwaye Tumaini Murungu.
Akizungumza katika Ukumbi wa Maji uliopo maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam ambapo sherehe za ndoa zilifanyika, Mushi alisema
alipotangaza nia ya kumuoa Tumaini baadhi ya ndugu zake walimtenga
lakini hakukata tamaa kwani aliendelea na taratibu za ndoa.
“Nilimpenda sana Tumaini na niliamini ndiye mwanamke wa maisha yangu
lakini nilipowaambia ndugu zangu kuwa nataka kumuoa, baadhi walinitenga
kwa uamuzi wangu huo wa kumuoa Tumaini ambaye ni mlemavu wa ngozi eti
nitakuwa nimeleta balaa nyumbani.
“Nilimuomba Mungu anisaidie na nikaongea na waumini wenzangu ambao walikubali kunifanyia sherehe.
Nawashukuru sana wakwe zangu ambao walinipokea na kunipa ushirikiano
katika kulitimiza tukio hili. Pia nimshukuru mama yangu kwani uwepo wake
umenipa faraja kubwa,” alisema Mushi.
Wakizungumzia kitendo cha Mushi kutengwa na baadhi ya ndugu zake, baadhi
ya waumini walilaani wakieleza kuwa, si jambo zuri hata kidogo.
“Inaumiza sana, unajua binadamu wote ni sawa, kwani msichana albino
hastahili kuolewa? Tuache ubaguzi usiyo na maana ambao unamchukiza hata
Mungu.
"Eti kuoa albino ni mkosi kwenye familia, nani kasema? Imani hizi potofu
zikemewa kwa nguvu zote,” alisema muumini mmoja aliyejitambulisha kwa
jina la Eliza.
CHANZO GLOBAL PUBLISHERS
0 comments:
Post a Comment