Dar es Salaam. Wiki iliyopita nilibahatika
kuhudhuria Tamasha la Watoto wa Mitaani ambalo liliandaliwa na Shirika
la ‘Hope for the Children’ maalumu kwa ajili ya kutafuta vipaji vya
uimbaji na uigizaji.
Ilikuwa ni sherehe ya aina yake kati ya zile
ambazo nimewahi kuzishuhudia. Kutokana na shauku ya kutaka kujua mengi
kutoka kwa watoto hawa kwanza nilivutiwa zaidi na aliyeonekana kuwa
mdogo kuliko wote.
Kwa kuwa tamasha hilo lilikuwa linafanyika katika
eneo la wazi na kulikuwa na kelele nyingi, nilimwomba mhusika mmoja
katika maeneo hayo aniruhusu niingie ukumbini kwa ajili ya kuzungumza na
mtoto huyu.
Mtu huyo aliniambia ‘dada ningependa sana
kukuruhusu ufanyie mazungumzo humu ndani, lakini hawa watoto hawaamiiki
wanaweza kuiba kitu chochote hivyo ninachoweza kukusaidia ni kukupa viti
tu, lakini mazungumzo mkafanyie nje’.
Ukiuliza hadithi za watoto wa mitaani kila mtu
atakwambia anayoifahamu, zipo za kusikitisha, kufurahisha na kufundisha
na hii ni moja kati ya hizo.
Katika maisha ya kawaida inapofika saa 11:00
alfajiri, familia nyingi huanza siku kwa kuamka na kujitayarisha tayari
kukabiliana na pilika za siku nzima. Wazazi au wasaidizi wa ndani
huwaamsha watoto kwa ajili ya kujiandaa kwenda shuleni.
Watoto huandaliwa kifungua kinywa wakati mwingine
hulazimishwa kula ili washibe kwa kuwa shibe ni moja ya nguzo muhimu
katika kutafuta elimu.
Kupata elimu, kulindwa, kutotumikishwa na
kuthamini ni haki za msingi ambazo watoto wote duniani wanapaswa
kuzipata na anapozikosa hizi ndiyo mwanzo wa kuzaliwa kwa watoto wa
mitaani.
Nilizungumza na mtoto huyu aitwaye Madilu Ngonyani
(12) ambaye katika umri huo pamoja na kuishi mtaani ana jukumu zito la
kuitunza familia yake.
Swali la kwanza nililomuuliza ni kwa nini yupo
mtaani kwa kuwa katika umri wake alipaswa kuwa shuleni, naye alinijibu
akisema hajui kwa nini mpaka wakati huo mjomba wake hajamwanzisha shule
ingawa mara kwa mara amekuwa akimpa ahadi hizo.
Ananisimulia sababu ya kuwa pale katika kundi la
watoto wa mitaani akisema kuwa baba yake alimwacha kwa mtu ambaye ndiye
sasa anayemwambia kuwa ni mjomba wake.
Hakumbuki lini alianza kuishi mitaani isipokuwa
anasema baba yake anayemtambulisha kwa jina moja tu la Ngonyani
alimwacha kwa mtu huyo akisema anarudi kijijini kwao mkoani Ruvuma
kulima.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment