Mamlaka ya Mapato Tanzania iko katika msuguano na
wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na mamlaka hiyo
kuanzisha mfumo mpya wa utoaji stakabadhi za kielektroniki kwa kutumia
mashine ziitwazo EFD.
Ugomvi mkubwa wa wafanyabiashara hao unatokana na
bei inayodaiwa ni kubwa ya kununulia mashine hizo, inayofikia Sh800, 000
kwa kila moja. Madai mengine ni kasoro za kiufundi za mashine hizo na
kitendo cha TRA kutumia mzabuni mmoja kuingiza mashine hizo.
Jana mvutano huo ulipiga hodi katika eneo maarufu
kibiashara la Kariakoo jijini Dar es Salaam ambapo wafanyabiashara
waligoma kufungua maduka kama ambavyo wamekwishafanya wenzao katika
mikoa ya Mbeya na Morogoro.
Pamoja na ufafanuzi wa TRA kwamba baada ya
majadiliano na wafanyabiashara bei za mashine za EFD zimepungua hadi
Sh600, 000 kwa kila moja, bado muafaka kamili haujafikiwa.Tunaafikiana
na ushauri unaotolewa na TRA kwamba mvutano huo umalizwe kwa amani kwa
njia ya mazungumzo na majadiliano baina ya mamlaka hiyo na
wafanyabiashara badala ya njia waliyoichagua ya migomo na maandamano.
Tunaishauri TRA iendelee kutoa majibu sahihi na
kusisitiza umuhimu wa mashine hizo, huku ikitambua kwamba hakuna
mfanyabiashara anayelipa kodi akicheka, hivyo iwe imara kusimamia mfumo
huo mpya bila kuingiza ujanja ujanja unaoweza kuikwamisha.
Kinachojitokeza bayana hapa ni kuwapo mawasiliano
hafifu baina ya TRA na wafanyabiashara. Kwa mfano, wafanyabiashara bado
wanadhani ni kampuni moja tu iliyopewa tenda ya kusambaza mashine hizo,
wakati ni kampuni 11 zilizopewa tenda hiyo. Hakika, tatizo ni
mawasiliano na TRA lazima ikiri udhaifu huo na kuchukua hatua stahiki.
Uanzishaji wa mashine za EFD ni mkakati sahihi wa
ukusanyaji na usimamizi wa kodi, hasa katika maeneo ambayo TRA haikuwa
inayafikia. Ni uamuzi ambao utaliwezesha Taifa letu kupata fedha za
kutosha kujenga miundombinu na kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi
na kijamii.
Tunashawishika kuamini kuwa, hata mafanikio ambayo
TRA iliyaeleza wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Mlipakodi ya kuimarika
kwa ukusanyaji mapato kutoka Sh4,049.1 trilioni mwaka 2008/09 hadi
Sh7,739.3 trilioni mwaka 2012/13, yamesaidiwa na mashine hizo.
Kwa muda mrefu tumekuwa tukikemea uzembe na
usimamizi mbovu wa kodi uliosababisha maofisa wa TRA kuacha fedha nyingi
zikilala kwa wafanyabishara wa kati, badala yake kila kukicha wakawa
wanakimbilia makusanyo ya kuokota yanayotokana na mishahara ya
wafanyakazi.
Kwa mfano, tumewahi kushauri kuwa vinahitajika
vyanzo vipya vya mapato, kwa kuwatambua na kuwatoza wafanyabiashara wa
kada ya kati katika maduka, baa, saluni, bucha za nyama, kumbi za
starehe na harusi na maeneo kama hayo.
Mbali na kuongeza mapato, pia tunadhani Serikali
ingefanya juhudi za kuziba matundu na mianya ya uvujaji wa mapato yake
ili kuhakikisha kila kinachokusanywa kinaelekezwa katika maendeleo ya
nchi na wananchi, badala ya kutafunwa na mchwa wasiojali masilahi ya
umma.
Hatuna shaka kwamba TRA ikijipanga inaweza
kukusanya mapato zaidi, hasa ikisimamia vizuri uamuzi wake wa kutumia
EFD nchini kote na kuweka utaratibu wa kudumu wa kufuatilia kwenye
maduka kuona iwapo wanatoa risiti hizo au la, maana tayari kuna madai
kuwa wateja wanatakiwa kuchagua kati ya kuuziwa bidhaa kwa bei ndogo
bila risiti au kwa bei kubwa na risiti za kielekroniki.
Chanzo;Mwananchi.
Chanzo;Mwananchi.
0 comments:
Post a Comment