“Nilifika na baba hapa alinichukua toka Mwanza akaniambia ananileta kwa shangazi anayeishi hapa kuja kusoma” anasema Cosmas.
Hebu tafakari, kijana wa miaka 12 ambaye hajawahi kufika jijini Dar es
Salaam, anafika Ubungo kwa mara ya kwanza akiwa na baba yake, na ghafla
wanapotezana.
Hii ilimtokea kijana, Cosmas Steven, 13 ambaye alifika hapa jijini mwezi
Januari akitokea Mwanza yeye pamoja na baba yake. Baada tu ya kufika
katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo, Cosmas alipotezana
na baba yake.
“Nilifika na baba hapa alinichukua toka Mwanza akaniambia ananileta kwa shangazi anayeishi hapa kuja kusoma” anasema Cosmas
Kwa bahati mbaya, Cosmas hakuweza kumpata baba yake na matokeo yake,
aliishia kuishi katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam ambapo kwa sasa
anaishi kwa kuuza chupa tupu za maji na kucheza kamari.
Cosmas ambaye ameishia darasa la sita anasema: “Natamani kurudi nyumbani
na kumuona baba yangu lakini sielewi namna ya kumpata, nnachojua ni
kuwa anaitwa Steven John”
Cosmas pamoja na watoto wengine wa mitaani katika eneo hili wanaishi
maisha yasiyo na utofauti na wanyama. Wanaoga katika Mto wa Msimbazi
nyakati za usiku wakati watu wote wamelala.
Wanalala katika vibaraza vya maduka katikati ya jiji ambapo hata hivyo
hutakiwa kuchangia gharama ya malazi ya shilingi 200 hadi 300 kwa usiku
mmoja.
Chanzo chao kikuu cha mapato ni kuuza chupa tupu zinazozagaa kwa wenye
viwanda na kampuni ambazo zinanunua chupa hizo kwa kilo na kucheza
kamari au kuombaomba pembezoni mwa barabara.
Hata hivyo, fedha hizo wakati mwingine huenda zisiwe riziki kwao kwani
usiku wanapolala vibaka au watoto wa mitaani wenye nguvu zaidi yao,
huwanyang’anya kwa nguvu fedha hizo.
Haya ndiyo maisha ya watoto wa mitaani ambapo si Cosmas pekee bali lipo
kundi kubwa la vijana wanaoishi mitaani Tanzania nzima.
Tovuti ya Humanium Help the Children(HHC) inaeleza kuwa katika Jiji la
Dar es Salaam pekee kuna watoto 3,000 hadi 5,000 ambao wanaishi
mitaani.
Pia tovuti hiyo inaeleza kuwa watoto hao wengi wao wana umri wa kuanzia
miaka mitano hadi 18 ambapo asilimia 80 kati yao ni wanaume wenye umri
wa miaka saba hadi 14.
Mkurugenzi wa Elimu kwa Watoto, kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kuhudumia Watoto,(Unicef) Dk Victoria Masabo anasema tatizo la watoto
wa mitaani linaendelea kuwa kubwa na gumu kwa sababu kadhaa ikiwemo
wazazi na walezi.
“Wazazi na walezi ndiyo watu wa kwanza wanaotakiwa kuhakikisha kuwa
mtoto anaishi salama, kuhakikisha yupo wapi na anafanya nini,’ anasema
Anasema talaka, kuvunjika kwa familia na migogoro ndicho chanzo kikubwa kinachosababisha ongezeko la watoto wa mitaani.
Anashauri kuwa taasisi zitafute njia mbadala kuhakikisha kuwa watoto wa
mitaani wanapata maeneo maalumu kwa ajili ya watoto hao na wahakikishe
wanakaa katika maeneo hayo, wanapata elimu hadi watakapokuwa watu
wazima.
Dk Masabo anasema tatizo hili la watoto wa mitaani lisipofanyiwa kazi
basi taifa litazalisha wezi, majambazi, makahaba na kizazi haribifu.
Ipo sheria Tanzania ambayo inaeleza kuwa iwapo polisi atamkuta mtoto wa
mitaani anayeonekana hana umiliki wa wazazi, basi atatakiwa amchukue na
kumpeleka katika taasisi.
Sheria ya watoto ya mwaka 2009 inakataza watoto kuzagaa mitaani na iwapo
wataonekana mitaani basi sheria hiyo inasema wanatakiwa kupelekwa kwa
ofisa ustawi wa jamii.
Afisa ustawi wa jamii anatakiwa afuatilie iwapo mtoto au watoto hao wana
wazazi na kama hawana wazazi basi watafutiwe wazazi mbadala na kama hao
pia hawatapatikana basi watoto hao wapelekwe katika vituo maalum au
taasisi.
Kwa bahati mbaya, sheria hii haifuatiliwi na wanajamii au hata na polisi
watunza sheria, na matokeo yake watoto wa mitaani wanakosa haki zao na
furaha ya utoto wanayotakiwa kuipata.
Gazeti la Mwananchi lilijaribu kumpigia simu Waziri wa Wanawake, Jinsia
na Watoto, Sophia Simba pamoja na naibu wake kwa mchango wao hawakuweza
kupatikana.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment