WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi
zitakazonufaika katika masuala ya uwekezaji nchini endapo itatekeleza
kikamilifu Mapitio ya Mfumo wa Uwekezaji yaliyowasilishwa na Taasisi ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD).
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Januari 31, 2014), wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuzindua kitabu cha Mapitio ya Mfumo wa Uwekezaji kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu Pinda alisema kuwa malengo ya mapitio
ya mfumo huo ni kuboresha hali ya uwekezaji na biashara nchini ambayo
matokeo yake yatasaidia kuongeza wawekezaji katika maeneo mengi.
“Kuna
maeneo ya uwekezaji yanayopata uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya
nchi (Foreign Direct Investment -FDI) ambayo ni umeme, mafuta, gesi,
madini, viwanda, ujenzi na huduma za jamii.”
Amesema
kuwa matokeo ya jitihada hizi ni makubwa na yameonekana ndani ya miaka
miwili tu. Akitoa mfano, alisema: “Kilimo kimeweza kukua kutoka dola za
marekani milioni 304.5 mwaka 2010 hadi dola za marekani milioni 355.4
katika mwaka 2011. Vilevile kwenye sekta ya Umeme na Gesi imekua kutoka
dola za kimarekani milioni 328.6 hadi dola za kimarekani 539.8 mwaka
2011.”
Kutokana
na matokeo hayo, Waziri Mkuu ameeleza kuwa Tanzania ina fursa nyingi
zikiwemo rasilimali, nafasi yake kijiografia na historia ya siasa safi
ambazo zinaifanya iwe kivutio kikubwa cha uwekezaji. Hali hiyo Waziri
Mkuu alisema, imesaidia Pato la Taifa kuendelea kukua kwa asilimia sita
kwa miaka 10 mfululizo na mwaka jana ilikua kwa asilimia saba na sasa
inatarajiwa kufika asilimia 7.2 kwa mwaka huu.
Miongoni
mwa maeneo yanayohusishwa na mfumo huu wa mapitio ya Uwekezaji ni yale
yaliyoainishwa katika Matokeo makubwa sasa ambayo ni Kilimo, Maji,
Uchukuzi, Elimu na Nishati.
“Ili
kufanikisha maeneo hayo ni muhimu tukajenga mazingira bora ya
uwekezaji, hivyo Serikali inawataka wadau wote kwa kushirikiana na Sekta
binafsi kuchambua kwa makini mapendekezo ya mapitio ya mfumo huo ambayo
yanatumika pia kuharakisha mafanikio ya Matokeo makubwa sasa”,
alisisitiza Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu alisema Serikali ya Tanzania inashukuru sana Taasisi ya
Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) kwa kuweka sura maalum
kwenye kitabu hicho inayozungumzia changamoto za uwekezaji kwenye sekta
ya kilimo na jinsi ya kukabiliana na changamoto hizo.
“Ninatumaini
kuwa utekelezaji wa mapendekezo haya utaongeza ufanisi wa mchakato huu
na kuhakikisha kuwa tunazitumia fursa zilizopo na nyingine zaidi katika
kuboresha uwekezaji katika kilimo nchini. Na kwenye kilimo ninamaanisha
kilimo mazao, mifugo, uvuvi na nyuki,” aliongeza.
Mapema,
Naibu Katibu Mkuu wa Taasisi ya OECD, Bw. Rintaro Tamaki, alisema
mazingira ya uwekezaji nchini yanabadilika kila mara kutokana na
kuvumbuliwa kwa rasilimali mpya kama vile gesi, makaa ya mawe ambazo
zinasababisha watu wavutive kuwekeza nchini.
”Kutokana
na kugunduliwa na sekta hizo, Serikali isizipuuzie sekta za zamani
hususan Sekta ya kilimo, cha msingi ni kuboresha sekta hii kwa kuanzisha
viwanda ili kuongeza thamani ya mazao yenu”.
IMETOLEWA NA:OFISI YA WAZIRI MKUU,S. L. P. 3021,DAR ES SALAAM.IJUMAA, JANUARI 31, 2014
0 comments:
Post a Comment