Home » » Kesi ya Madabida yapigwa kalenda

Kesi ya Madabida yapigwa kalenda

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida.
 
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeahirisha kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na wenzake watano ya usambazaji wa dawa bandia za Kupunguza Makali ya Virusi vya Ukimwi (ARVs) na kuisababishia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) hasara ya zaidi ya Sh. milioni 148.3 hadi Machi 18, mwaka huu itakapotajwa tena.
Hatua hiyo ilifikiwa jana baada ya upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Mwanaisha Kombo, kudai kuwa kesi hiyo ilipangwa kutajwa jana lakini upelelezi wake haujakamilika.

Hakimu Mkazi Nyigulila Mwaseba, alisema kesi hiyo itatajwa tena Machi 18, mwaka huu na dhamana ya washtakiwa inaendelea.

Mbali na Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha kutengeza dawa cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPIL), Madabida, washtakiwa wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora wa Dawa wa MSD, Sadiki Materu.

Wengine ni Meneja Uendeshaji, Seif Shamte, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye pia ni Meneja Masoko, Simon Msoffe, Mhasibu Msaidizi wa MSD, Fatma Shango na Evans Mwemezi.

Februari 10, mwaka huu, Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro, aliwasomea kwa mara ya kwanza mashitaka yao matano likiwamo linalomkabili Madabida, Shamte, Msoffe na Shango, kwamba Aprili 5, mwaka 2011, jijini Dar es Salaam, waliuza na kuisambazia MSD makopo 7,776 ya dawa bandia aina ya Antiretroviral kwa nia ya kudanganya.

Ilidaiwa kuwa pamoja walijipatia Sh.148,350,156.48  kutoka kitengo cha MSD wakidai fedha hizo ni malipo ya dawa halisi aina ya ‘Antiretroviral’ wakati wakijua siyo kweli.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washtakiwa wote walikana.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa