Rais Jakaya Kikwete amesema uteuzi wa majina 201 ya wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba umekamilika na kati ya leo na kesho,
atayatangaza pamoja na tarehe ya kuanza kwa Bunge hilo.
Bunge la Katiba litakalokuwa na wajumbe 640,
litakutana kwa siku 90 kujadili Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Desemba 30, mwaka jana.
“Bunge la Katiba litakutana katika wiki ya tatu ya
mwezi huu. Mambo yanayosubiriwa ni mawili tu, uteuzi wa wajumbe 201 na
siku ya kuanza kwa Bunge hili. Mambo haya yote ninayesubiriwa
kuyakamilisha ni mimi tu,” alisema Rais Kikwete alipokuwa akihutubia
katika kilele cha maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa CCM.
Alisema kazi ya uteuzi wa wajumbe hao ilikamilika
tangu juzi na kinachofanyika sasa ni kuhariri majina hayo na kurekebisha
mambo kadhaa.
“Jumatatu (leo) tutayapitia majina haya ili tuone
kama tunaweza kurekebisha. Baada ya hapo tutaweza kutangaza na inaweza
kuwa siku hiyohiyo au kesho yake (Jumanne), hazitazidi siku hizi mbili,”
alisema.
Alisema hivi sasa ukarabati katika Ukumbi wa
Bunge, Dodoma bado unaendelea na mkandarasi ameeleza kwamba hadi
Februari 10, mwaka huu atakuwa amemaliza kazi.
“Nimewapa siku tano hadi saba za kujaribu spika na
vipaza sauti ili kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa, lakini pia
nitakwenda kupata ushauri wa wanasheria ili kuweza kutangaza siku ya
Bunge hili kukutana,” alisema.
Amshangaa Mbowe
Katika hotuba yake Rais Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa CCM, alimshangaa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa
kauli yake kwamba mfumo wa Serikali tatu ukikataliwa katika Bunge hilo,
nchi haitatawalika.
“Huku ni kuwadanganya wananchi, pale hakuna ngumi
wala vurugu yoyote, kila ibara iliyopo katika rasimu itajadiliwa ili
upatikane mwafaka. Huku ni kukosa ukomavu wa kisiasa,” alisema.
Alisema si kweli kwamba kila mwanaChadema anataka
mfumo wa Serikali tatu na kila mwanaCCM anapendelea mfumo wa Serikali
mbili akisema kinachohitajika ni ushawishi wa kujenga hoja ili
wanaopinga wakubaliane.
Chanzo;mwananchi
Chanzo;mwananchi
0 comments:
Post a Comment