Sophia Simba naye afunguka
Mwanasiasa mkongwe nchini, mzee Kingunge Ngombale-Mwiru.
Pia ameonyesha masikitiko yake dhidi ya baadhi ya viongozi wakuu wa CCM kuwaumbua na kuwadhalilisha baadhi ya mawaziri kwa kuwaita 'mizigo'.
Kingunge alisema hayo alipozungumza na NIPASHE juzi nyumbani kwake, jijini Dar es Salaam, alisema haoni tatizo kwa Lowassa na hata mwanachama yeyote ndani ya CCM kujitokeza na kuonyesha dhamira ya kutaka uongozi mapema.
Alisema kujitokeza mapema kwa mtu mwingine yeyote mwenye dhamira ya kutaka uongozi ni jambo litakalowasaidia wananchi kuwafahamu, kuwajadili na kuwapima kwa kina kuona kama wanafaa kuongoza au la.
Hivyo, akasema haoni sababu ya kuibuka malumbano baina ya wanaCCM au kusakamwa kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwa kauli yake inayotafsiriwa kuwa ameonyesha nia ya kuutaka urais mwakani kupitia CCM.
Alisema wengine wanaotaka kufanya hivyo wafanye ili kutoa nafasi kwa wanachama wenzao na wananchi kwa jumla kuwafahamu na kuwajadili ili ukifika wakati wa uchaguzi wajue la kufanya dhidi yao.
“Sipendi kuingia kwenye malumbano na wanachama wenzangu kwa sababu najua mwishowe watu tunaweza kuvuana nguo. Ila kwa mtazamo wangu sioni kama ni kosa kwa wanachama na raia yeyote mwenye nia ya kutaka uongozi kujitokeza na kujionyesha mapema,” alisema.
Alionyesha: “Kujitokeza kwao mapema kutawafanya wananchi wawaone, wawafahamu, pia wawapime na kuwajadili kwa kina kama wanafaa kubeba majukumu ya uongozi au la. Pia sidhani kama ni Lowassa pekee aliyefanya hivyo. Vipi asakamwe yeye tu? Siyo dhambi watu wenye nia iwe katika ubunge, udiwani, uenyekiti wa serikali za mitaa na hata urais kuwangong’oneza rafiki na ndugu zao juu ya dhamira yao. Bora hao kuliko wanaofanya mambo yao kwa usiri,” alisema Kingunge.
Kingunge, ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ukiwamo uwaziri katika serikali za awamu zote nne nchini tangu enzi za Mwalimu Nyerere, alisema tangu enzi za chama cha Tanu mpaka kuzaliwa kwa CCM, upo msisitizo unaosema raia wote wana haki mbili kuu ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa, ingawa hawalazimishwi.
“Hakuna anayelazimishwa kuchagua au kuchaguliwa kwa maana ya kuwania uongozi. Hivyo, kujitokeza kwa wanasiasa na watu wengine kuonyesha nia yao ya kutaka uongozi hawafanyi dhambi. Hivyo, sidhani kuna haja ya suala hili kuwa mjadala mkubwa wakati kuna mambo ya msingi, ambayo CCM inapaswa kuyazungumza na kuyajadili kwa kina kwa manufaa ya wananchi,” alisema Kingunge.
Juu ya kitendo cha viongozi wakuu wa sekretarieti ya CCM kufanya ziara mikoani kisha kutangaza majukwaani majina ya mawaziri walioitwa mizigo, Kingunge kwanza alipongeza ziara hiyo akidai itasaidia kukijenga na kuinua uhai wa CCM.
Lakini alidai hakubaliani na kilichofanywa na viongozi wao kuwavua nguo watendaji hao wa serikali.
Alihoji ina maana viongozi wa CCM hawajui mipaka ya uongozi iliyopo baina yao na serikali iliyopatikana kwa ridhaa ya wananchi?
“Zipo taratibu za kukosoana ndani ya chama. Mawaziri ni wabunge. WanaCCM kama wamefanya makosa ilipaswa waitwe na kukosolewa katika vikao vya ndani ya chama badala ya kuwavua nguo hadharani kwa kisingizio wananachi ndiyo wanaowalalamikia. Haya hatukuwatuma,” alisema Kingunge.
Alisema yapo mambo ya msingi viongozi wa CCM wanapaswa kuyazungumza na kuyajadili mbele ya wananchi, ikiwamo mikakati ya kuwaletea maendeleo ili wafurahie uhuru.
Pia alisema kwa miaka mingi tangu enzi za Tanu, CCM ilifahamika kuwa ni chama cha wanyonge, lakini akasema kwa sasa hilo halipo na kuwataka viongozi kuhakikisha wanaliangalia na kukirejesha chama katika mstari.
“Kama wameshindwa kazi ni vyema wakawapisha wengine wakiongoze, kuliko kukiyumbisha chama na kukifanya kipoteze mvuto mbele ya wananchi kwa kujadili mambo yasiyo na maana kwa wananchi hata kama wanapigiwa makofi. CCM ina sera na taratibu zake za kukosoana kupitia vikaoni, siyo kilichofanywa na viongozi wetu,” alisema Kingunge.
Alisema viongozi wa CCM kwa sasa ni kama wanaoanzisha vita baina yao na watendaji wa serikali, kitu ambacho siyo tu kinaonyesha chama chao kuyumba, bali kinaonyesha pia namna gani wanavyofanya kazi ya kuwasaidia wapinzani badala ya kujijenga na kusaidia serikali yao ili waje kushinda katika chaguzi zijazo.
Alihoji viongozi waliowaita wanachama wenzao 'mizigo' ndani ya serikali inayotokana na CCM wanatazamanaje na mawaziri hao waliorejeshwa.
“Sidhani kama ni jambo zuri. Watu waheshimu mipaka ya madaraka yao. Wajikite katika kukijenga chama na serikali kwa jumla, badala ya vitu visivyo na tija kwa wananchi iliyowapa ridhaa ya kuongoza,” alisema Kingunge.
SIMBA AONYA WANACCM WANAOPIGANA ‘MAWE’
Nao Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa CCM umewaonya wanachama walioanza kupigana ‘mawe’ kwenye mbio za urais kipindi wanapoteza muda wao na kuwataka kuacha tabia hiyo ukisema mashindano yao yatakivuruga chama.
Mwenyekiti wa UWT, Sophia Simba, alitoa msimamo huo juzi wakati akizungumza katika mahojiano na NIPASHE iliyotaka kujua maoni ya Umoja huo katika suala la urais wa 2015 ndani ya CCM.
Simba, ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, alisema asilimia 98 ya watu wanaozungumzia masuala ya urais kipindi hiki wana makundi yao, ambayo ni hatari, kwani yatakivuruga chama.
“Ukishaona saa zote watu wanaropokaropoka kuhusu urais ujue hao wana makaundi yao. Sisi kama UWT tunawataka waache kuropokaropoka, waache kupigana mawe, wanazungumzia masuala ya urais kipindi hiki wana interest (maslahi) zao,” alisema Simba.
Kwa mujibu wa Simba, chama kimetulia, hivyo wanaotaka kukivuruga ni wanachama wenye makundi yao.
Hata hivyo, alisema mashindano yao hayatakitisha chama, kwani wanapoteza muda kuzungumzia masuala hayo wakati inafahamika muda haujafika. Alisema kwa upande wa kina mama wametulia kimya, hawazungumzii masuala ya urais, kwani wanapoteza muda wao wakati haujafika wa kuanza kuzungumzia masuala ya urais.
“Sisi kina mama tumetulia kama maji ya kwenye mtungi. Unaona kina baba na uzee wao wanajitokeza na kuzungumzia masuala ya urais sababu ya makundi yao ya urais,” alisema Simba.
Tangu mwaka jana kumekuwa na malumbano makali yanayokwenda sambamba na kupigana vijembe ndani ya CCM, yakilenga makundi na watu wanaodaiwa kuwa na nia ya kuwania urais mwakani.
Malumbano hayo yamekwenda mbali zaidi kwa kuwahusisha wapambe wao hali, ambayo imekifanya chama kutokuwa na utulivu.
Mlengwa mkuu katika malumbano haya ni Lowassa akiwa ametajwa na Katibu wa Uenezi na Chipukizi wa Jumuiya ya Vijana wa CCM, Paul Makonda na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Tanzania Bara, John Malecela ambao kwa nyakati tofauti wamemshutumu kwamba anakigawa chama kwa kuanza kampeni mapema na kutumia fedha.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment