Mshtakiwa Makongoro Joseph Nyerere anayekabiliwa na kesi ya
mauaji ya kukusudia ya mfanyabiashara wa madini, Onesphory Kituli,
ameutaka upande wa mashtaka kuwa wazi kuhusu upelelezi wa kesi yao na
iwapo jalada lao kama lipo kwa DPP ama kwa RCO.
Mbali na Makongoro mwingine anayekabiliwa na kesi
hiyo ya mauaji ya kukusudia ni mfanyabiashara maarufu wa Dar es Salaam,
Abubakar Marijan (50) maarufu kwa jina la Papaa Msofe.
Makongoro alitoa malalamiko hayo jana mbele ya
Hakimu Mkazi, Hellen Liwa baada ya Wakili wa Serikali,Leonard Challo
kudai upelelezi wa kesi bado haujakamilika.
Baada ya Wakili Challo kutoa maelezo hayo,
Makongoro aliiambia mahakama kuwa wanataka kufahamu upelelezi wa kesi
yao umefikia wapi na kuhoji kuwa, awali upande wa mashtaka ulisema
jalada hilo la kesi yao tayari lipo kwa DPP na jana kwa RCO.
Alihoji ni kwa nini upande wa mashtaka hawataki
kuwa wakweli kuhusu kesi yao. Hakimu Liwa alimwambia kuwa sawa
wamemsikia na kuahirisha kesi hadi Februari 18, 2014 kwa ajili ya
kutajwa na kuamuru washtakiwa kupelekwa rumande kwa sababu shtaka lao
halina dhamana.
Papa Msofe alipandishwa kizimbani kwa mara ya
kwanza peke yake Agosti, 2012 na kusomewa shtaka la kumuua Kituli kwa
makusudi, kinyume cha kifungu cha 196 cha Kanuni za Adhabu sura ya 19
kama kilivyorekebishwa mwaka 2002.
Makongoro aliunganishwa na Papa Msofe katika kesi
hiyo, Februari 13,2013. Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kulitenda
kosa hilo,Oktoba 11, 2011 nyumbani kwake, Magomeni Mapipa.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment