Home » » Sumatra yakamata daladala 307 Dar

Sumatra yakamata daladala 307 Dar

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa nchi Kavu na Majini (Sumatra)
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa nchi Kavu na Majini (Sumatra) Kanda ya Mashariki, imesema kamatakamata iliyofanywa Januari, mwaka huu imefanikiwa kunasa daladala 307 mkoani Dar es Salaam kutokana na makosa mbalimbali likiwamo la kushindwa kutoa tiketi kwa wanafunzi.
Lengo la operesheni hiyo ni kusimamia na kudhibiti  vitendo viovu vya ukiukwaji wa taratibu za usafiriji ili kuwafanya wamiliki, madereva na makondakta wa magari yanayotoa huduma ya usafiri jijini Dar es Salaam kuwa makini.

Kati ya magari 307  maarufu kama daladala yaliyokamatwa,146 yalipatikana na kosa la kufanya biashara ya usafirishaji bila ya leseni hususani katika maeneo ya pembezoni mwa Jiji kama Kivule na Gongo la Mboto.

Mengine 46 yalikuwa yakiiba ruti kwa lengo la  kuongeza nauli, 41 yalikatisha ruti, 23 kupandisha nauli kwa abiria, 31 kuchanganya sare kwa madereva na makondakta, tisa kutoa lugha chafu na 11 kushindwa kutoa tiketi kwa abiria.

Ofisa Mfawidhi wa Sumatra Kanda ya Mashariki, Conrad Shio, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam juzi.

Shio alisema inapobainika kosa limetendeka, mmiliki ama dereva anapaswa kulipa faini ya Sh. 100,000.

Aidha, alifafanua kuwa kama itabainika udanganyifu wa tiketi kutoka katika ruti tofauti faini yake ni Sh. 200,000.

“Ni haki ya msingi kwa wanafunzi kupatiwa tiketi kama ilivyo kwa abiria wengine, hakuna sheria ya kumnyima mwanafunzi tiketi na ikibainika hatua zitachukuliwa,” alisisitiza Shio.

Aidha, alisema kisheria wanapswa kushirikiana na vikosi vyote ndani ya Jeshi la Polisi wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Hivyo alisema kwa sasa wanashirikiana na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kwa ajili ya kuhakikisha magari yote yanayokamatwa yanafikishwa kwenye yadi.

Alisema awali walikuwa wakifanyiwa fujo na wapiga debe wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo, lakini baada ya kukishirikisha kikosi hicho hali hiyo sasa imedhibitiwa.

Mohamed Juma, kondakta wa daladala inayofanya safari zake kutoka Gongo la Mboto kwenda Posta, alisema alifikishwa katika ofisi za Sumatra baada ya kukamatwa kwa kosa la kuchanganya sare na hivyo alilazimika kulipa faini ya Sh. 250,000.

Hata hivyo alilalamika kuwa kiasi hicho ni kikubwa mno.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa