Kiongozi Mstaafu wa CCM, Pius Msekwa
Kiongozi Mstaafu wa CCM, Pius Msekwa amesema
endapo vyama vya upinzani vikiungana na kuweka mikakati makini ya muda
mrefu, vinaweza kuking’oa CCM madarakani.
Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na mwandishi
wetu jana, Msekwa alisema kwa mtindo wa sasa wa vyama vya upinzani kila
kimoja kusimama peke itakuwa ndoto kukishinda CCM.
“Kama vyama vya upinzani vinataka kuwe na upinzani
wenye nguvu dhidi ya CCM ni lazima viungane vyote. Tena viweke
mikakakati ya muda mrefu ya kujiimarisha,” alisema Msekwa kwenye
mahojiano hayo.
Hata hivyo, alisema kuiondoa CCM madarakani siyo
kazi rahisi kwa sababu mizizi yake imeenea kila kona ya nchi huku
akisema wazo la upinzani kuungana halitakuwa rahisi kwa kuwa wengi wao
ni walafi wa madaraka na hakuna atakayekuwa tayari kuvunja chama chake
na kuunda kimoja kwa hofu ya kukosa uongozi.
Akijibu swali kuhusu nguvu ya Chadema kwa sasa
Msekwa alisema: “Wanapambana na CCM kwenye majukwaa ya kisiasa lakini si
kuwa na watu wengi wanaokiunga mkono.”
Alisema CCM kina mizizi hadi ngazi za chini kabisa nchi nzima tofauti na vyama vingine.
Alisema Chadema kiko katika baadhi ya maeneo ya
Tanzania Bara wakati Zanzibar hakina nafasi, tofauti na CUF ambacho
alisema angalau kinaonyesha kuwa na nguvu visiwani huko.
Kuhusu Chadema kuwa na wabunge wengi Tanzania
Bara, Msekwa alisema ni neema iliyokiangukia baada ya CCM kufanya makosa
ya uteuzi kwa baadhi ya majimbo.
Msekwa ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge alisema pamoja na neema hiyo, Chadema hakiwezi kufikia asilimia 40 ya wabunge wote.
“Kweli Chadema kimejitahidi lakini ukichunguza
utabaini ni neema iliyowaangukia kutokana na makosa ya CCM kuteua watu
ambao wapigakura walikuwa hawawataki,” alisema Msekwa.
Alisema Chadema kimekuwa kikionekana kufanya
vizuri kwenye siasa za majukwaani kwa sababu kina nafasi kubwa ya
kukosoa na hata kutoa madai ya kutunga dhidi ya CCM ili mradi yawe
yanawagusa wananchi.
Kuhusu uwezekano wa vyama vya upinzani kuchukua
nchi kutokana na CCM kuwa na makundi mengi ambayo yanaweza
kukisambaratisha katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 Msekwa alisema:
“Hakuna mtu anayeweza kuondoka CCM na kuivunja nguvu. Hata akiwa ni
kiongozi mwenye nguvu ya kisiasa kiasi gani ataondoka mwenyewe na CCM
kubaki imara.”
Alitoa mfano wa wanasiasa maarufu kama Oscar Kambona
aliyejiuzulu mwaka 1967 na kukawa na hofu ya wananchi kuandamana lakini
haikuwa hivyo.
Pia alimtaja aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya
Ndani, Naibu Waziri Mkuu na baadaye Waziri wa Kazi, Augustine Mrema
ambaye alihama CCM na kuonekana kuwa na nguvu kubwa kupitia chama cha
NCCR kwenye uchaguzi wa mwaka 1995.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment