Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi
Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye (kulia), akizungumza na waandishi wa
habari (hawako pichani), kuhusu semina ya `Think Big' ambayo itafanyika
siku ya Alhamisi wiki hii jijini Dar es Salaam. Walengwa wa semina hiyo
ni wawekezaji wazawa, wamiliki wa biashara na wajasiriamali ambao
wanapenda kufikiria na kufanya biashara zao katika wigo mpana zaidi.
Pamoja naye ni Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Dk. Reginald Mengi (katikati)
na Mkurugenzi wa Uanachama, Louis Accaro.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa TPSF, Godfrey Sembeye, alisema, semina hiyo inatarajiwa kufanyika kesho kutwa huku mgeni rasmi akiwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu.
Alisema, lengo kuu la semina hiyo ambayo ni maandalizi ya mkutano wa kimataifa wa masuala ya uwekezaji unaotarajiwa kufanyika nchini Novemba 24, mwaka huu, kuwa ni kuihamasisha sekta binafsi kufikiri katika uwanja mpana zaidi kwa kuanzisha mpango mkubwa wa kuapanua wigo wa kuwa na mitaji ya ubia na binafsi.
Naye Mwenyekiti wa TPSF, Dk. Reginald Mengi, aliwataka Watanzania kufikiri mambo makubwa katika biashara zao na kwamba ukombozi wa nchi hauwezi kuja bila ule wa kiuchumi.
Kuhusu wawekezaji wa nje kuja kuwekeza nchini, Dk. Mengi, alisema, uwekezaji wa ndani na wa nje ni wa muhimu na kwamba kama kuna mtu anakataa wawekezaji wa nje, atakuwa hana ufahamu sawa sawa ila wanaporuhusiwa, maslahi ya Watanzania yazingatiwe kwanza.
Kwa mujibu wa Sembeye, takribani washiriki 200 hadi 300 wanatarajiwa kuhudhuria semina hiyo kwa kiingilio cha kati ya Sh. 200, 000 kwa wanachama wa TPSF na 300,000 kwa walio nje ya taasisi hiyo.
Baadhi ya walengwa wa semina hiyo ni pamoja na wawekezaji, wamiliki wa biashara, wajasirimali ambao ni wazawa, wajumbe wa bodi wakiwamo, wakurugenzi watendaji wa wanachama takribani 200 kutoka TPSF, watendaji na maafisa watendaji kutoka taasisi za biashara, benki za maendeleo, mifuko ya pensheni ya jamii na kampuni za bima na zile zinazohusika na utoji wa huduma au biashara katika taaluma ya sheria pamoja na washauri wa huduma za kitaalamu.
Wengine ni maafisa watendaji wa taasisi za serikali zinahusika na masuala ya uwezeshaji kiuchumi na uwekezaji kama vile taasisi ya Financial Sector Deepening Trust (FSDT), Baraza la Taifa la Uwezeshaji wa Kiuchumi (Neec), Mamlaka ya kushughulikia Michakato ya Uuzaji bidhaa Nje ya nchi (EPZA), Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Soko la Mitaji na Hisa (CMSA), Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na Taasisi ya Kukuza Viwanda Vidogovidogo nchini (Sido).
Alitaja walengwa wengine kuwa ni maafisa watendaji wa mitaji ya ubia na mitaji binafsi wa taasisi za aina hiyo zilizopo nchini na Mtanzania, majasiriamali pamoja na taasisi za vyuo vikuu za biashara na wanataaluma.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment