Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Ameonya kwamba sheria haiwezi kumhurumia mtumishi anayekiuka kanuni na taratibu za utumishi.
Waziri Nyalandu amefikia hatua hiyo kufuatia taarifa zinazohusiana na ukiukaji wa kanuni na taratibu za utoaji wa vibali baada ya ofisa wanyama pori wilayani Meatu, Mohammed Omary, kudaiwa kufanya kosa hilo.
Omary, analalamikiwa na baadhi ya wananchi wa vijiji vya Mwangudo, Iramba Ndogo na Makao inavyozunguka hifadhi ya kijamii WMA ya Makao, kutoa vibali vya kuua wanyama kipindi ambacho msimu umefungwa.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusiana na madai hayo, Omary alisema vibali hivyo vinatolewa kwa ajili ya kitoweo kwa watu wa kabila la Watindiga na si vinginevyo.
Alisema kimsingi sheria inazuia kufanya shughuli za uwindaji katika mapori ya hifadhi za wanyama baada ya msimu kufungwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, George Wanga, alipoulizwa kuhusu suala la utoaji wa vibali vya uwindaji katika WMA ya Makao kipindi ambacho msimu umefungwa alisema hakuwa na taarifa.
“Kwa kweli sijui lolote kuhusu suala hilo, na kama kweli hayo yanafanyika huko Makao, ofisi yangu haijatoa baraka za kufanya hivyo," alisema Wanga.
SOURCE:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment