Home » » Tafiti sera ya filamu yaiva

Tafiti sera ya filamu yaiva

Shirikisho la Filamu Tanzania TAFF, pamoja na vyama vingine vinane  vinavyounda umoja huo jana wamewasilisha utafiti  wa sera ya filamu nchini kwa Wizara ya Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo Rais wa TAFF, Simon Mwakifwamba alisema, wanaiomba serikali kuwaunga mkono katika rasimu hiyo ambayo wameifanya kwa juhudi zao binafsi, ikiwa ni pamoja na kutafuta mdhamini wa kuwawezesha katika kufanya utafiti huo uliochukua siku 20.
Akizungumza kwa ufupi juu ya utafiti huo, Mwakifwamba alisema,  katika utafiti wao waligundua endapo serikali itapitisha rasimu hiyo ajira kwa vijana, uchumi, utalii vitakua kwa sababu kwa kupitia filamu nchi inaweza kutangazika kitaifa na kimataifa.
Mambo mengine yaliyoibuliwa katika utafiti hu,o ni pamoja na tasnia ya filamu kuhusisha wizara kadhaa ikiwamo Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Fedha, Wizara ya Utalii, Wizara ya Viwanda na Biashara hivyo endapo wataweza kufanya kazi pamoja tasnia hiyo itakua, pamoja na kukuza uchumi kwa jumla, alisema Mwakifwamba.
“Tunaiomba serikali  kwa kupitia utafiti huu tuliyoifanya ilete changamoto kwao  na waifanyie kazi,  haya maoni ya wadau ambayo yametolewa , sisi hatuhitaji fedha  tunahitaji mazingira mazuri ya kufanya kazi, kwani tangu tuanze tumekuwa tukifanya kazi bila dira ya kutuongoza katika kazi zetu, wakiipitisha tuna imani kubwa tutaweza kufanikiwa vyema pamoja na kazi zilizo bora,” alisema Mwakifwamba.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa  tafiti hiyo, Mkurugenzi Idara ya Sera na Ushirikiano wizarani hapo Joyce Mwakisyala alisema, “Kama Wizara  tumepokea utafiti  huu ambao  unaainisha  maoni ya wadau  ambao wameshirikishwa  katika kujadili na kuleta maendeleo katika filamu nchini.
“Wizara inajipanga katika  kuifanyia kazi  sheria  ikiwamo COSOTA na ile ya bodi ya filamu ambayo hivi sasa imepitwa na wakati. Hivi sasa serikali tunaandaa sera ya tasnia ya utamaduni  ikiwamo kuzingatia masuala ya maadili katika sanaa,” alisema Mwakisyala
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa