Home » » Polisi yamshikilia shabiki mmoja

Polisi yamshikilia shabiki mmoja

Shabiki mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi akidaiwa kukutwa na tiketi bandia kwenye mechi ya Ligi Kuu ya kati ya Yanga na Mbeya City iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, Boniface Wambura alisema jana kuwa Matei Cosmas (28) ambaye ni mkazi wa Buza Njiapanda Kitunda, Dar es Salaam amefunguliwa jalada namba CHA/IR/900/2014 kwenye Kituo cha Polisi Chang’ombe akidaiwa kupatikana na tiketi bandia.
“TFF jana asubuhi ilifika katika Kituo cha Polisi Chang’ombe kusaini hati ya maelezo dhidi ya mtuhumiwa.
Ni imani ya Shirikisho kuwa mtuhumiwa atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchini.”
Wambura alisema tunatoa mwito kwa washabiki wa soka kuepuka kununua tiketi kutoka mikononi mwa watu, kwani kufanya hivyo ni kosa. Tiketi zinauzwa kwenye sehemu maalumu zenye chapa ya TFF.
Katika hatua nyingine, Wambura alisemaTFF imepokea kwa masikitiko kifo cha aliyekuwa mchezaji wa Vijana, Moro United na Yanga, Omari Changa kilichotokea Februari mosi, jijini Dar es Salaam.
“Msiba huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu kwani Changa wakati wake uwanjani akichezea timu mbalimbali alitoa mchango mkubwa ambao tutaukumbuka daima.
“TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Changa, klabu ya Moro United na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Katika maziko TFF itawakilishwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Kidao Wilfred, na imetoa rambirambi ya sh. 200,000.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa